RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema hatua za makusudi zinapaswa kuchukuliwa ili kuzuia na kupunguza madhara yanayotokana na maafa.
Dk. Mwinyi aliyasema hayo, katika uzinduzi wa nyumba za maafa katika Kijiji cha Nungwi kilichopo Mkoa wa Kaskazini Unguja na nyingine zilizopo Tumbe Mkoa wa Kaskazini Pemba, ambazo zilijengwa kwa ajili ya wananchi walioathiriwa na mvua za masika mwaka 2017.
Katika maelezo yake, Rais Dk. Mwinyi alisema miongoni mwa hatua zinazopaswa kuchukuliwa ni kuendeleza mipango miji, ambayo inabainisha sehemu za ujenzi wa makazi, mabondeni, maeneo ya kilimo, ujenzi wa miundombinu ya barabara na huduma za jamii.
“Ni vyema tukahakikisha tunakuwa na ‘Master Plan’ (mpango mkuu) kwa kila mji tunaojenga, ili kuweka mifumo na utaratibu mzuri wa kupambana na maafa,” alisema Rais Dk. Mwinyi.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi alieleza kuwa ujenzi wa nyumba hizo umelenga kuimarisha maisha ya wananchi baada ya kupatwa na maafa.
Rais Dk. Mwinyi alisema maafa na majanga yamekuwa yakijitokeza katika nchi zote duniani kwa namna mbalimbali ambapo hakuna nchi iliyoweza kuwa na teknolojia ya kuzuia majanga na maafa yasitokee.
Alisema hata nchi zilizoendelea hupata taharuki kubwa zinapokumbwa na maafa kama vile vimbunga, tsunami, matetemeko ya ardhi, mafuriko, moto na mengineyo.
Kwa upande wa Zanzibar, Rais Dk. Mwinyi alisema hatua zinaendelea kuchukuliwa ikiwemo kuanzisha Kamisheni ya kukabiliana na maafa kupunguza athari za maafa kwa maisha ya watu na mali zao kwa kuchukua hatua madhubuti za kujikinga, kujitayarisha, kukabiliana na kurudisha hali ya kawaida ya maisha ya wananchi baada ya maafa kutokea.

Aliongeza Kikosi cha Zimamoto na Uokozi Zanzibar, vimepewa mafunzo maalumu ya kukabiliana na kutoa misaada wakati wa maafa na kuwepo mifumo ya utabiri wa hali ya hewa inayosimamiwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania ambayo ni taasisi ya Muungano.
Pamoja na hayo, Rais Dk. Mwinyi aliwahimiza wananchi waliopewa nyumba hizo wazitunze vizuri, wadumishe usafi katika eneo lote hilo na waishi kwa kuzingatia misingi ya upendo, udugu na ujirani mwema.
Rais Dk. Mwinyi alitoa shukurani kwa Ofisi ya Ubalozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu nchini Tanzania na kupongeza kazi nzuri inayofanywa na Balozi Khalifa Abdulrahman Almarzouqi, Balozi wa (UAE) nchini pia, alitoa shukurani kwa meneja wa mradi huo kwa kazi nzuri aliyofanya na kumpongeza mshauri elekezi na mkandarasi kwa kufanikisha mradi huo.
Naye Kaimu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi Saada Mkuya alisema familia 54 ambazo zina idadi ya watu 261 Unguja na Pemba, wanaishi katika vijiji hivyo ambapo pia, wanafunzi wa maandalizi na msingi 277 wanasoma katika vijiji hivyo wakiwemo 151 Nungwi na 126 Tumbe.
Na MWANDISHI WETU, Zanzibar



























