WATANZANIA na Waganda wanatarajiwa kufurahia na kunufaika zaidi na uhusiano wa kihistoria kati ya nchi hizo, kutokana na mipango ya kufungua uwekezaji mkubwa na vitegauchumi vya kibiashara.
Neema hizo ni utekelezwaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ukiwemo ujenzi wa Bomba la Mafuta kutoa Hoima Uganda hadi Tanga, Tanzania, Tanzania kufungua Ofisi ya Bandari Uganda, ujenzi wa kiwanda cha chanjo na miradi ya barabara kuunganisha hizo mbili.
Akizungumza wakati wa Dhifa ya Kitaifa baada ya mapokezi ya Rais Yoweri Museven wa Uganda, Rais Samia Suluhu Hassan, alisema katika mazungumzo yao, wamekubaliana kwa pamoja kuondoa vikwazo visivyo vya kikodi vilivyokuwa vinakwamisha biashara baina ya mataifa hayo.
Rais Samia alisema hatua hiyo itaongeza wigo wa biashara baina ya mataifa hayo huku akieleza kwamba, tayari wameshawaagiza mawaziri wa kisekta wa pande zote kukutana kuzungumzia hayo.
Kwa mujibu wa Rais Samia, Uganda ni nchi ya pili kwa Afrika Mashariki inayoongoza kuwekeza Tanzania ambapo mwaka huu Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kimesajili miradi 45 kutoka nchi hiyo yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 114 na ajira 2,150.
Alisema vivyo hivyo Tanzania imewekeza nchini Uganda, kwamba ni imani yake ziara hiyo ya Rais Museveni itafungua zaidi milango ya fursa za uwekezaji na kufungua ushirikiano zaidi.
“Nilipomwambia kuhusu kiwango cha biashara baina yetu alisema it’s a shame ‘Ni aibu’ kwa maana ni kidogo hivyo kuna haja ya kukiongeza,” alisema.

Alitaja takwimu za bidhaa zilizosafirishwa kutoka Tanzania kwenda Uganda zina thamani ya sh. bilioni 439.8, mwaka jana kutoka bilioni 121 mwaka 2014.
Rais Samia alisema mataifa hayo yamekuwa na ushirikiano katika miradi mbalimbali, ukiwemo wa Bomba la Mafuta kutoka Hoima Uganda hadi Tanga Tanzania.
Pia, alisema Rais Museveni ameridhia Tanzania kujenga Ofisi ya Bandari ya Dar es Salaam katika Jiji la Kampala, ili kuongeza idadi ya mizigo katika bandari hiyo.
“Kuna moja zuri sijalisema la kutumia Bandari ya Dar es Salaam, mizigo imeongezeka lakini si kwa kiwango cha kuridhisha sana, ili kuongezeka nikamuomba aturuhusu tuweke ofisi ya Bandari pale Kampala, naye akanambia njooni kesho wala msichelewe,” alisema.
Alisema ofisi hiyo itawarahisishia wafanyabiashara wa Uganda kuwasiliana na Tanzania na hivyo, kuongeza idadi ya mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam.
Rais Samia alisema wamekuwa na mazungumzo mazuri yenye kuamsha matumaini ya mashirikiano kwa siku zijazo na ni muendelezo wa mambo yaliyokubaliwa wakati wa mtangulizi wake, Hayati Dk. John Magufuli.
HISTORIA YA UNDUGU
Alieleza uhusiano baina ya mataifa hayo unatokana na mambo matatu ambayo ni; undugu, historia na jiografia.
Rais Samia alifafanua matunda ya ushirikiano huo ni juhudi za pamoja za kupiga vita dawa za kulevya na mambo mengine ambayo yamekuwa chachu ya kuimarika kwa amani za mataifa hayo.
Hata hivyo, alitoa pole kwa Rais Museveni kutokana na milipuko iliyosababisha vifo na majeruhi kwa raia wa Uganda, akisema Tanzania ipo bega kwa bega na taifa hilo.
MKUTANO WA WALI
Awali, akizungumza Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Samia alisema kwa pamoja wamekubalina kushirikiana kujenga kiwanda cha chanjo ya magonjwa mbalimbali, kwa wanyama na binadamu.
Kwa upande wake Rais Museveni alisema uhusiano na ushirikiano baina ya mataifa hayo ulianza muda mrefu tangu harakati za Uhuru wa mataifa hayo.
Rais Museveni alisema hiyo ni hatua ya pili ya ushirikiano na hasa unahusisha kuboresha mataifa kwa kuwa tayari yana watu walioelimika na rasilimali muhimu.

Alimpongeza Rais Samia kwa hatua ya kuifanya Uganda kuwa nchi ya kwanza kutembelea baada ya kutwaa wadhifa wa urais.
Aliuelezea mradi wa bomba la mafuta, kwamba utapeleka mafuta katika mataifa mengine ya Afrika na hivyo, kudumisha biashara baina ya mataifa hayo na kusema ana farijika kuwa Tanzania kwani ni nyumbani kwake.
“Waafrika walikuwa wamelala, kwa sababu kuna utajiri katika maradhi, mtu ukiumwa mwenzio anakupatia dawa anapata pesa, sisi tumeanza harakati za kuwekeza katika upatikanaji wa chanjo na dawa kwetu,” alisema.
Aliyataja mambo mengine waliyozungumza ni usafiri, mifugo na umeme huku akisisitiza kwamba jambo muhimu katika yote ni soko, jambo ambalo wanatarajia kulizungumza leo.
Wakuu hao wa nchi leo, watafungua kongamano la biashara litakalowakutanisha wadau kutoka Tanzania na Uganda, sekta binafsi ili kujadili fursa za biashara kati ya mataifa hayo.
NA JUMA ISSIHAKA



























