BAADA ya Lugha ya Kiswahili kutengewa Julai 7 kila mwaka kuwa siku rasmi ya kuadhimishwa duniani, serikali imesema hatua hiyo inakuja na fursa lukuki za kupanuka soko la ajira za ualimu kimataifa na utalii wa utamaduni wa Tanzania.
Aidha, wabobezi na wanazuoni wa Kiswahili nchini, wamesema mafanikio hayo yawe chachu ya kuweka mkazo katika matumizi ya lugha na usahihi wake, pia kuandaa mikakati ya ufundishaji.
Akizungumza na UhuruOnline, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk, alisema hatua hiyo ni fursa kwa Watanzania.
FURSA ZENYEWE
Naibu Waziri Nassor, alizitaja fursa hizo ni kuitangaza nchi, utamaduni wake na hivyo kuvuta watalii watakaotamani kuona mahali ilipozaliwa lugha ya Kiswahili.
Balozi Nassor alibainisha faida nyingine ni kufunguka kwa soko la ajira ya ualimu wa lugha hiyo kwa mataifa mbalimbali duniani.
“Kwa sababu Kiswahili kitatambulika na ulimwengu wote, bila shaka mataifa mengi yatahitaji kujifunza lugha hii, hakuna mahali watakapopata walimu zaidi ya Tanzania, hivyo tutapara ajira,” alisema.
Hata hivyo, alieleza baadhi ya nchi ambazo Tanzania ina soko kubwa la ajira ya ualimu wa Kiswahili kwa sasa ni Afrika Kusini na Jamhuri ya Demokrasi ya Congo.
Kwa upande wake, Mhadhiri wa Kiswahili wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk. Boniface Alphonce, alisema kitendo cha Kiswahili kutengewa siku rasmi ya kuadhimishwa ni hatua nyingine mbele katika maendeleo ya lugha hiyo.
Dk. Alphonce alisema kupitia azimio hilo la Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni Duniani (UNESCO), Kiswahili kinafungua ukurasa mwingine na kwamba, hiyo itasababisha ongezeko la mataifa yatakayohitaji kujifunza lugha hiyo duniani.
“Kiswahili kwa sasa ni lugha ambayo inapanua mawanda yake, kwahiyo hii ni fursa tunapaswa kujivunia na tuendelee kukipigia chapuo tuone kwamba Kiswahili kimeshavuka mipaka na kuwa bidhaa,” alisema.
Alisema ili kuendelea kuiishi lugha hiyo na fursa zake za sasa, kila Mtanzania anapaswa kuweka mkazo katika matumizi ya lugha na usahihi wake, pia kuweka uwezekano wa kukiingiza katika matumizi ya kitaaluma.
Kwa mujibu wa Dk. Alphonce, ni tamanio la wadau wa Kiswahili kukiona kikitumika kufundishia masomo yote, ili kuongeza uelewa kwa wanafunzi kwa kuwa lugha hiyo inaeleweka zaidi na Watanzania.
“Tukiitumia hii fursa kama tumeingia huko badi nasi tuandae mikakati ya kukiweka katika nyanja za ufundishaji, lakini sisi wadau tumepokea kwa furaha, tumechukulia kama fursa nyingine kwa lugha hii na tunapaswa kukipigania,” alifafanua.
Profesa Aldin Mutembei ni Mhadhiri wa Kiswahili, Idara ya Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema hatua hiyo inachangia katika kuongeza wingi wa lugha zinazotambulika ulimwenguni.
Alisema duniani kuna lugha sita ama saba zilizotengewa siku maalumu na Kiswahili kinakuwa lugha ya kwanza Afrika.
Profesa Mutembei aliyataja mambo mengine muhimu kutokana na hatua hiyo; ni kukua kwa utamaduni wa Tanzania na kuongeza hamasa ya ufundishaji wa lugha hiyo kwa kuwa wanaofundisha watajivunia kutumia lugha inayotambulika kimataifa.
Alisisitiza, ili kuendana na hali hiyo ni muhimu watu kuacha tabia ya kudharau vyakwao, huku akiishauri serikali kufanya uwekezaji katika vifaa vya kujifunzia na kufundishia lugha hiyo.
Naye Mhadhiri wa Kiswahili wa UDOM, Dk. Eguine Sanga, alisema maadhimisho hayo ni moja ya njia za kuitangaza lugha hiyo ulimwenguni na hivyo itakua na kuenea.
Alisema kwa kuwa Kiswahili kitasikika masikioni mwa watu, wengi watapata kiu ya kukijua na hapo ndipo soko la ufundishaji litakapofungukia.
Dk. Sanga alishauri Watanzania kujikita katika kufanya utafiti, kuandika vitabu na majarida mbalimbali ya kuonyesha ubora na thamani ya lugha ya Kiswahili.
Kwa mujibu wa Dk. Sanga, jukumu jingine ni kuwaandaa wataalamu watakaosambazwa katika mataifa mbalimbali kufundisha lugha ya Kiswahili.
AZIMIO LA UNESCO
Kiswahili kimepata hadhi hiyo kupitia UNESCO, ambalo limeipitisha Julai 7 ya kila mwaka kuwa siku ya kuadhimisha lugha ya Kiswahili duniani.
Hatua hiyo inakifanya Kiswahili kuwa lugha pekee kutoka Bara la Afrika kupewa siku yake maalumu ya utambulisho na kuadhimishwa.
NA JUMA ISSIHAKA



























