JESHI la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limelaani vitendo vya baadhi ya wananchi kujipatia fedha kwa udanganyifu wakidai kuwapatia vijana nafasi za kujiunga na jeshi hilo.
Pia limesema wadanganyifu hao wanatumia jina la Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venence Mabeyo na baadhi ya viongozi waliopo madarakani.
Akitoa tamko hilo Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa JWTZ, Luteni Kanali Gaudentius Ilonda, amesema udanganyifu huo umekuwa kero kwa wazazi, walezi na JWTZ.
Luteni Kanali Ilondo alisema shughuli za jeshi zinaendeshwa kwa kanuni na sheria na si wananchi kuamua wanavyotaka.
“Nawaomba Watanzania wapuuze udanganyifu unaofanywa kwa sababu hakuna nafasi kwa vijana kuingia jeshini kwa kutumia mgongo wa fedha,”alisema Luteni Kanari Ilondo.
Mbali na udanganyifu, alisema baadhi ya wananchi wanakwenda katika ofisi zao kuwaombea watoto wao kujiunga na jeshi hilo jambo ambalo si sawa.
“Jeshi lina taratibu zake, mtu huwezi kukurupuka kwenda jeshini kuomba nafasi ya kujiunga na jeshi ni lazima utaratibu ufuatwe,” alisema.
Ameongeza kuwa si kijana yeyote anayeruhusiwa kujiunga na jeshi, kwa kuwa lazima awe na sifa stahiki awe raia wa Tanzania wa kuzaliwa, amefikisha umri wa miaka 18 -28, afya njema ya mwili na akili timamu, nidhamu, hajawahi kushitakiwa sehemu yeyote, awe na cheti cha shule na kuzaliwa.
“Kazi ya jeshi ni ngumu na hatarishi, kama kijana ameingia kwa njia ya rushwa ya fedha hawezi kumudu kwasababu mazoezi yake ni magumu yanaweza kukupotezea uhai,”alisema.
Alisema jeshi linaandikisha vijana baada ya kupata idhini kutoka serikalini ambapo hadi sasa baadhi wanachukuliwa kujiunga na jeshi hilo baada ya viongozi wa nchi kutembelea baadhi ya miradi ya mkakati iliyopo ndani ya jeshi hilo.
“Viongozi wa serikali baada ya kuridhishwa na miradi wameamua kuongeza vijana wachache waliopo katika kambi za jeshi ili kuongeza nguvu zaidi katika miradi hiyo,”alisema Luteni Kanali Ilondo.
Na REHEMA MAIGALA