ELIMU na uhamasishaji kwa jamii kuhusu huduma za lishe bora inayotakiwa kwa watoto wadogo katika malezi na makuzi, inahitajika ili kuondoa tatizo la udumavu nchini, imeelezwa.
Aidha, uelewa mdogo wa lishe umetajwa kuchangiwa na wazazi kutojua namna sahihi ya ulaji unaofaa kwa watoto.
Ofisa Lishe Mkoa wa Katavi, Asnath Mrema alieleza hayo alipozungumzia umuhimu wa lishe bora kwa watoto, ambapo alisema kula kwa mazoea kunachangia mtoto kupata udumavu kutoka na kukaririshwa kula vyakula vya aina moja bila ya kuwa na mchanganyiko wa virutubishi vya lazima ikiwemo kalori, protini, mafuta, wanga, vitamini na madini.
Pia, alisema mila na desturi potofu ni miongoni mwa sababu za watoto kuwa na udumavu kwa kutopewa baadhi ya vyakula kama mayai, nyama, samaki huku akisema hilo linatokana na wazazi kudhania kuwa vyakula hivyo vinaweza kuwaletea watoto madhara.
“Kuna baadhi ya wazazi wanawanyima watoto wao mayai eti wakila nywele hazitaota au wakila samaki hawatakuwa na akili, huo ni upotoshaji, hivyo niwasihi wazazi kuwapatia watoto wao vyakula vyenye virutubisho kadri wanavyoendelea kukuwa,” alisema Asnath.
Mhudumu wa Afya wa Kituo cha Afya Mwangaza, Hakia Mvungi, ambaye anawahudumua wajawazito, alisema kukosa chakula cha kutosha na mtoto kukaa na njaa kwa muda mrefu au kushiba bila kujali uwiano wa virutubishi, ni miongoni mwa sababu za mtoto kupata utapiamlo.
Aliongeza kuwa, udumavu hutokea kati ya siku moja tangu kutungwa kwa mimba hadi siku 1,000, hivyo mama mjamzito anatakiwa kupata lishe bora ili kurutubisha afya ya mwili wake na kiumbe aliyeko tumboni.
Asia Mbwana, Mhudumu wa Kliniki ya wajawazito na watoto katika Kituo cha Afya Amec, kilichopo Mtaa wa Madukani, Manispaa ya Mpanda, aliitaka jamii kuboresha namna ya ulishaji wa watoto wachanga na wadogo, pia alishauri kunyonyesha kwa kuzingatia utaratibu kwani kunapunguza viwango vya utapiamlo na vifo kwa watoto.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Dk. Omar Sukari alisema kuwa maradhi ya kuambukiza kama homa ya matumbo, nimonia na malaria huongeza mahitaji ya lishe, hivyo endapo mtoto atakosa huishia kupata utapiamlo.
Pia, Dk. Sukari alishauri kutolewa elimu ya lishe kwa jamii kupitia vyombo vya habari vya ndani na nje ya mikoa, mikutano ya hadhara pamoja na vituo vya kutolea huduma za afya.
Taasisi mbalimbali zikiwemo mashule, pia zinatakiwa kupatiwa elimu ili kuboresha lishe za watoto wawapo shuleni.
Na IRENE TEMU, Katavi



























