NI mechi ya hesabu! Simba ikiwa na mpango wa kupata pointi tatu ili kujiweka katika mazingira mazuri, katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara wakati Geita Gold ikitaka ushindi ili kujinusuru katika janga la kushuka daraja.
Simba leo itaikaribisha Geita Gold katika mchezo wa raundi ya saba, utakaopigwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba ipo nafasi ya pili kwa pointi 14 wakati Geita Gold ikiwa nafasi ya 13 kwa pointi tano wakati timu zote zikiwa zimeshacheza mechi sita kila moja.
Akizungumza Dar es Salaam, Kocha Msaidizi wa Simba, Selemani Matola, alisema wachezaji wake wapo vizuri na kasi yao ni ile ile ambayo walionyesha katika mchezo uliopita.
Alisema wamerekebisha baadhi ya mapungufu yaliojitokeza na sasa timu yao ipo vizuri na imejiandaa kuondoka na pointi tatu muhimu katika uwanja wa nyumbani.
“Kikosi kipo vizuri na wachezaji wote wapo fiti, isipokuwa Chriss Mugalu ambaye atakosa mchezo wa leo kutokana na majeruhi ambapo anaendelea na matibabu, tutapambana ili kuhakikisha tunapata pointi tatu ambazo ni muhimu kwetu,” alisema Matola.
Nahodha Msaidizi wa timu hiyo, Gadiel Michael, alisema wao kama wachezaji wamejipanga vizuri kuhakikisha wanaendeleza kasi walioanza nayo katika mchezo dhidi ya Ruvu shooting.
Alisema wachezaji wote wana ari kubwa ya mchezo huo na kila mmoja atatimiza majukumu yake akiwa dimbani.
Naye Kocha Msaidizi wa Geita Gold, Choki Abeid, alisema wamefuata pointi tatu katika mchezo huo na kwamba Simba wasitarajie kupata mteremko.
Alisema wanajua Simba ipo vizuri na ina kikosi cha wachezaji wenye ubora, lakini na wao wana wachezaji ambao walishawahi kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara hapo awali, hivyo wanatambua jinsi ya kukabiliana nao.
“Tunajua kasi yao na tumeshazisoma mbinu zao, hivyo hatuwahofii kwani na sisi tuna wachezaji ambao wana uzoefu na ligi,” alisema.
Nahodha wa Geita Gold, Geofrey Manyasi, amesema wachezaji wamejipanga vyema kuibuka na ushindi katika mchezo huo ili kujitoa katika nafasi ya chini waliyopo.
Na NASRA KITANA