KANDA saba zenye jumla ya wanamichezo 665 wameshiriki katika mashindano ya Umoja wa michezo na sanaa kwa vyuo vya ualimu nchini (UMISAVUTA) yaliyoanza jana mkoani hapa.
Mashindano hayo ambayo yamefunguliwa rasmi katika viwanja vya Nangwanda Sijaona na Naibu waziri wa elimu, sayansi na teknolojia, Pauline Gekul, kwa niaba ya Waziri Profesa Joyce Ndalichako, yanatarajia kumalizika Desemba 5, mwaka huu.
Naibu katibu mkuu wizara ya elimu, sayansi na teknolojia, Profesa James Mdoe, alisema kuwa mashindano hayo yanajumuisha michezo ya soka, netboli, mpira wa kikapu, wavu, mikono, riadha, sanaa za maonyesho, maigizo, ngoma, ubunifu, usafi na nidhamu.
Jumla ya washiriki ni 882 ambapo kati yao ni washiriki kutoka timu 7 za kanda za mashariki magharibi, kaskazini, kusini, kati na nyanda za juu kusini na Vyuo vilivyoko katika kanda hizo viliteua timu ambazo zilishindana huko kisha zikapatikana timu kwa kila kanda.
Washiriki wengine 217 ni viongozi kutoka wizara ya elimu, sayansi na teknolojia, ofisi ya raisi tawalaza mikoa na serikali ya mtaa (TAMISEMI), viongozi kutoka mkoani na wilayani na wadau wengine.
Mashindano hayo yalizinduliwa rasmi na naibu waziri wa elimu, sayansi na teknolojia, Pauline Gekul kwa niaba ya waziri Profesa Joyce Ndalichako.
Akizungumzia suala la mamluki ambalo lilijitokeza katika mashindano ya UMISETA, Profesa Mdoe alisema wamejipanga na kwamba sio rahisi kwa sababu wachezaji wote wanajuana kwa vile walitokana na mashindano ya kikanda ndio wakapatikana waliokuja katika mashindano ya jumla.
“Tunawaomba wana Mtwara na maeneo ya jirani kuja kushuhudia vipaji vilivyopo, michezoni afya vile vile ni ajira” alisema Profesa Mdoe.
Mkurugenzi msaidizi wa elimu ya ualimu, Huruma Mageni alisema kwamba viwanja vingine vitakavyotumika kwa ajili ya mashindano hayo ni pamoja na viwanja vya chuo cha ualimu kawaida na vile vya chuo cha ualimu wa ufundi vilivyopo mkoani mtwara.
Afisa utamaduni wa mkoa wa Mtwara, Fatuma Mtandi ameiambia UhuruOnline kwamba wamepokea mashindano hayo kwa furaha kubwa.
“Washiriki ni zaidi ya 800 kwanza tutashuhudia burudani ya vipaji vyao lakini vìle vile wanamtwara tutafaidika kiuchumi kila mmoja kwa shughuli zake mfano wenye hoteli, wauzaji wa vinywaji na kadhalika’alisema Mtandi.
Na Mwandishi wetu