WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, amewaagiza viongozi wa wizara hiyo kuandaa ripoti itakayo ainisha idadi ya wastaafu wanaokabiliwa na changamoto ya kutolipwa stahiki zao baada ya kustaafu zinazotokana na wizara na wale ambao changamoto zao zinatokana na ucheleweshaji mifuko ya Pesheni kulipa mafao.
Waziri huyo alitoa maagizo hayo jijini Dodoma wakati akifungua kikao Cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Wizara hiyo.
Amesema wakipata ripoti hiyo wataona kama zipo changamoto zilizo nje ya uwezo wao ili wizara izibebe kama ajenda kuu na kuzitafutia ufumbuzi wa kina.
Waziri huyo amesema inafikirisha na inaumiza kuona mstaafu anamliza utumishi wake serikalini halafu hapati stahiki zake kwa wakati na kubaki akihangaika.
Amesema wapo wastaafu ambao wamekuwa wakikaa hata miaka mitatu bila kulipwa stahiki zao jambo ambalo halileti afya kwa wastaafu hao na ni lazima lipatiwe ufumbuzi.
Waziri akizungumzia sikukuu za mwisho wa mwaka ikiwemo Chrimas na Mwaka mpya amewasii watanzania kuwa makini na hasa wale wanaotumia vyombo vya Moto ili kupunguza ajali ambazo zimekuwa zikitokea kwa wingi kipindi hicho na kuathiri maaisha ya watanzania na Mali zao na kuleta vifo.
“Mwisho wa mwaka ni kipindi ambacho vyombo vya moto vinaongezeka barabarani ambapo watanzania wanasafiri kwenda huku na huko kwa ajili ya sikukuu hizo, kuna watu wanaingia barabarani ni malena kabisa na ukiwaangalia hata hawastahili kuendesha magari lakini kwa kuwa anataka kwenda kuonyesha ndugu jamaa na marafiki anaendesha, ….
“Ni vizuri kama hujui kuendesha ukatafuta dereva watu watajua tu kama gari ni yako,”amesisitiza Simbachaweni.
Kuhusu baraza la Wafanyakazi amesema ni chombo muhimu kinachounganisha muajiri na wafanyakazi katika kuainisha changamoto, hoja malengo na mafanikio kwa pamoja hivyo ni muhimu kuzingatia utaratibu wa kukutana kama sheria inavyotaka.
Naye Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Hamza Khamis Chilwa, amewataka watumishi hao kuwa na siri kama ambavyo maadili ya kazi yao yanataka hasa katika eneo la matumizi ya fedha, wahakikishe wanatoa taarifa za matumizi ya fedha katika eneo husika na si katika kila kikao jambo ambalo litasaidia kuondoa sitofahamu na fikra tofauti.
Pia amewaagiza kuimarisha na kuendeleza umoja na mshikamano miongoni mwao ili waweze kufikia malengo kama walivyokusudia kwani wasipofanya hivyo si rahisi malengo na matarajia yao kuyafikia.
Awali Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Christopher Kadio, amesema kikao hicho kinatanguliwa na viko vya baraza 6 ya wafanyakazi yaliyochini ya wizara hiyo ikiwemo Baraza dogo la Jeshi la Polisi nchini, Jeshi la Magereza, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na Mamlaka ya vitambulisho vya Taifa (NIDA).
Amesema pamoja na mafanikio mbalimbali ambayo wameyapata bado wanakabiliwa na changamoto katika utekelezaji wa majukumu yao ikiwemo suala la uko wa bajeti ambalo halikidhi mahitaji, Uhaba wa watumishi na vitendea kazi.
Na Happiness Mtweve,Dodoma



























