KATIKA kuhakikisha machiga wanapata mazingira stahiki ya kufanyia biashara Jiji la Dodoma limeingia Mkataba na Kampuni ya Mohamed Builder Limited kwa ajili ya Ujenzi wa Soko kubwa la Wamachinga ‘Open Market’ maarufu Machinga Complex eneo la Bahi road Jijini Dodoma.
Mradi huo unaotarajiwa kugharimu Sh. bilioni 4.9 katika awamu ya kwanza na litachukua wamachinga zaidi ya 2000 na utatumia muda wa miezi minne kuanzia sasa.
Akizungumza katika hafla ya utiliaji saini Mkataba wa ujenzi wa Soko hilo jijini humo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka amesema, dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuhakikisha Wamachinga wanakuwa na eneo la uhakika katika kukuza uchumi wao na Taifa kwa ujumla.
Mtaka amemtaka Mkandarasi wa Kampuni ya Mohamed Builder kuhakikisha anakamilisha Mradi wa ujenzi wa Soko hilo kwa muda uliopangwa pamoja na kuzingatia thamani ya pesa.
Naye Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru, amesema kuwa wanajenga soko hilo kwa mapato ya ndani na Serikali Kuu.
Mafuru amesisitiza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutakuwa na faida nyingi huku akiwahakikishia Wamachinga kutobughudhiwa tena katika eneo hilo.
“Ujenzi wa mradi huo ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha machinga wanakuwa na sehemu salama na stahiki kwa ajili ya kufanyia biashara zao na si kuzagaa zagaa kila mahali,”amesema Mafuru.
Awali Meya wa Jiji la Dodoma Profesa Davis Mwamfupe amesema lazima Machinga aheshimiwe kwani kazi hiyo ni kama kazi nyingine hivyo soko hilo linaleta hadhi ya Makao Makuu ya Nchi na Serikali.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mohamed Builder Limited, Taher Jaffery ameahidi kukamilisha Ujenzi huo kabla ya muda uliopangwa ili kukidhi mahitaji ya wananchi huku Mwenyekiti wa Wamachinga Mkoa wa Dodoma, Bruno Mponzi, ameishukuru Serikali kwa uamuzi wa kuwajengea Soko hilo kutokana na kuwajali.
Na Happiness Mtweve,Dodoma



























