MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafiri Aridhini (LATRA), imetangaza kuwatia mbaroni mawakala wawili na kuzibaini kampuni mbili za mabasi yaendayo mikoa ya Manyara na Mwanza, kwa tuhuma za kupandisha nauli.
Hatua hiyo imekuja ikiwa ni siku moja baada ya Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Mwita Waitara kufanya ziara ya kushtukiza katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli, Mbezi Jijini Dar es Salaam na kubaini ulanguzi wa nauli kwa mabasi yaendayo mikoani.
Wakati LATRA ikitangaza hayo, Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani, kimetangaza kung’oa namba za mabasi tisa yanayotoa huduma za usafiri Nyegezi, mkoani Mwanza, kutokana na ubovu.
Hayo yalijiri kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam na Mwanza, ambako wadau mbalimbali wa usafiri wakiwemo LATRA walikuwa wakikagua huduma za usafiri ili kuhakikisha wananchi wanasafiri bila ya vikwazo, kikiwemo cha ulanguzi wa tiketi.
Desemba 22, 2021, Uhuru ilifika katika kituo cha mabasi cha Magufuli na kufanikiwa kujionea hali halisi ya usafiri huku wadau wa usafiri wakiwemo LATRA wakizungumzia hatua zilizochukuliwa kuhakikisha abiria wanasafiri salama na nauli hazipandishwi kiholela.
Akizungumza na Uhuru, Mkurugenzi wa Udhibiti, Usafiri wa Barabara LATRA, Johansen Kahatano, alisema mamlaka hiyo ilianza ukaguzi kwa kila basi saa 10:00 alfajiri ya jana, katika kituo cha Magufuli.
Kahatano alibainisha kuwa kutokana na operesheni hiyo, walibaini uwepo wa changamoto kwa baadhi ya abiria, kushindwa kusema ukweli kiasi cha fedha walizolipa kutokana na kutishiwa kwamba endapo watasema, basi hawatasafirishwa, jambo linalowafanya wengine kuvumilia kulipa kiwango kikubwa cha nauli.
Mkurugenzi huyo alitoa rai kwa wananchi wanaotaka kusafiri kwenda mikoani kuhakikisha wanakata tiketi katika ofisi za kampuni za mabasi na kuhakikisha wanalipa nauli stahiki.
Kahatano aliwatahadharisha wamiliki wa mabasi kuwa waangalifu kwa kuwa ikibainika basi limetoza nauli tofauti na utaratibu, mmiliki wake atatakiwa kulipa faini ya sh. .200,000.
TABOA WAFUNGUKA
Kwa upande wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA), kimebainisha kwamba changamoto ya upandishaji holela wa nauli kipindi cha sikukuu, inatokana na kutokuwepo kwa watoa huduma.
Mkurugenzi wa Habari wa TABOA, Aboubakar Mwalongo, aliyasema hayo alipozungumza na Uhuru na kueleza kuwa suala hilo walishalifikisha kwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, lakini halijapatiwa ufumbuzi.
“Wapo watu wengi wanaofanya huduma humu ndani lakini hawana vitambulisho, jambo ambalo linatoa mwanya kwa utapeli huo, kwa sababu abiria wanashindwa kutambua wakala halali na asiye halali,” alisema na kutaja changamoto nyingine inayosababisha hali hiyo kuwa ni kukata tiketi katika vituo visivyo rasmi vilivyopo nje ya kituo hicho.
KAULI YA MENEJA
Meneja wa Kituo cha Magufuli, Mkama Maira, alisema wanaendelea kulifanyia kazi agizo la Naibu Waziri Waitara kwa kufuatilia na kuwalinda abiria ili wasipate usumbufu kwa wasafirishaji.
“Tunashirikiana na LATRA na TABOA kuhakikisha abiria wanasafiri vizuri bila bughuza yoyote. Katika kipindi chenye wasafiri wengi, ukweli ni kwamba kunakuwepo na baadhi ya watu wanaoleta ujanja ujanja wa kupandisha bei kwa siri,” alisema na kuwataka abiria kutoa ushirikiano kwa uongozi wa kituo hicho ili kuwabaini watu hao na kuwadhibiti.
“Abiria watoe taarifa ofisi zetu ziko wazi muda wote ili kuwahudumia wao, inapotokea wakafanyiwa vitendo kama hivyo vya kupandisha nauli tofauti na bei elekezi zilizoainishwa na LATRA, tuwachukulie hatua,” alisema.
Aliongeza kuwa wanapobaini kampuni imekiuka utaratibu wa nauli huwa wanaikabidhi kwa LATRA, ili kuchukuliwa hatua zaidi na kwamba ikitokea watumishi wa mamlaka hiyo hawapo huwa wanawapeleka Mahakama ya Jiji kwa kesi ya kubughudhi abiria, ambayo adhabu yake ni kifungo au faini kuanzia sh. 50,000.
Pia, alisema walifanikiwa kutekeleza agizo la Naibu Waziri Waitara kwa kulifuatilia basi lililokuwa linatoka Dar es Salaam kwenda Tabora, lililopakia abiria wa kwenda mikoa ya Tabora, Mwanza, Bukoba, Shinyanga na kuwatoza nauli tofauti na ile inayotakiwa, hivyo kulikabidhi kwa LATRA.
HALI ILIVYOKUWA
Katika kituo hicho, kulikuwa na umati wa abiria wakiendelea na utaratibu wa ukataji tiketi katika ofisi za kampuni mbalimbali za mabasi.
MABASI TISA YANG’OLEWA NAMBA
Desemba 22, 2021, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Kamishina Msaidizi wa Polisi, Wilbrod Mutafungwa, alisema wameng’oa namba za mabasi tisa katika stendi kuu ya mabasi ya Nyegezi, jijini Mwanza na kuyazuia kuendelea na safari, baada ya kubainika ni mabovu.
Akiwa katika stendi hiyo, Mutafungwa alisema idadi kubwa ya magari yamefanyiwa ukaguzi na askari wa kikosi hicho na mengine yanaendelea kukaguliwa.
“Kwa ukaguzi huo tumebaini ubovu wa magari hayo na hayataruhusiwa kubeba abiria mapaka pale yatakapokuwa yametengenezwa na kuhakikiwa usalama wa wake,” alisema na kutoa wito kwa wamiliki, mawakala na madereva kukutana ili kuwatafutia abiria usafiri mwingine.
SUPERIUS ERNEST NA IRENE MWASOMOLA



























