RAIS Samia Suluhu Hassan, amewashukuru viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kwa ushirikiano mkubwa na kuahidi Tanzania itashiriki kikamilifu katika kuhakikisha Jumuiya hiyo inatimiza malengo yake.
Aidha, alisema Tanzania ikiwa mwenyeji wa Makao Makuu ya EAC, itatoa ushirikiano, ili kuwezesha taasisi za Jumuiya kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Aliyasema hayo Desemba 22, 2021 Ikulu, Jijini Dar es Salaam, wakati akihutubia kwa mara ya kwanza Mkutano Maalumu wa 18 wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa EAC, uliofanyika kwa njia ya mtandao.
Katika kikao hicho kilichofanyika kwa njia ya mtandao, Wakuu wa Nchi na serikali wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walimkaribisha na kumpongeza Rais Samia kwa utendaji wake tangu ashike wadhifa huo.

PICHA NA IKULU
Pia, viongozi wa Jumuiya hiyo walisimama kwa dakika moja kumkumbuka Hayati Rais Dk. John Magufuli kwa mchango wake alioutoa kwa Jumuiya hiyo.
Mkutano huo, maalumu ulijadili ajenda kuu mbili ambazo ni kupokea ripoti ya Baraza la Mawaziri la Jumuiya hiyo ya uhakiki wa utayari wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kujiunga na EAC.
Ajenda ya pili ilihusu pendekezo la mabadiliko ya Kanuni ya 11(1) inayohusu akidi ya Mikutano ya Wakuu wa Nchi na Wanachama wa Jumuiya hiyo.
Wakuu wa Nchi wa Jumuiya hiyo, walipokea taarifa ya uhakiki na kuagiza Baraza la Mawaziri la EAC kuharakisha mchakato wa majadiliano ya mkataba yatakayowezesha DRC kuwa mwanachama na kuwasilisha taarifa hiyo katika mkutano wa kawaida utakaofanyika mapema mwakani.
Kuhusu ajenda ya pili iliyohusu Kanuni ya 11(1), Wakuu wa Nchi wa Jumuiya hiyo waliliagiza Baraza la Mawaziri la kisekta la Sheria na Mahakama kukutana.
Lengo la kukutana ni kujadili kuhusu pendekezo la mabadiliko ya Kanuni ya 11 (1) ya uendeshaji wa mikutano ya wakuu wa nchi, wanachama na kuwasilisha ripoti hiyo katika mkutano ujao wa kawaida wa wakuu hao kwa lengo la kujadili na kukamilisha suala hilo.
NA MWANDISHI WETU



























