WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima, amewataka Watanzania kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa virusi vya Corona, kuelekea mwisho wa mwaka.
Aidha, ameitaja mikoa mitano iliyofanya vizuri katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo huku akiwaonya wakuu wa mikoa mitano iliyofanya vibaya na iwapo hawana sababu za kufanya hivyo, ataitaarifa mamlaka ya uteuzi.
Dk. Gwajima aliyasema hayo jijini Arusha Desemba 22, 2021, wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Mpango Shirikishi na Harakishi kwa jamii, awamu ya pili dhidi ya Uviko-19.
Aliwakumbusha Watanzania kwamba ugonjwa huo upo na unaongezeka huku katika kipindi cha mwisho wa mwaka unaweza kusambaa kwa kasi endapo hazitachukuliwa hatua za kukabiliana na ugonjwa huo.
“Sisi wenyewe ndiyo tutaamua tufike mwaka mpya salama ama laa…,kazi ya serikali ni kuelimisha sio kushikana mashati,” alisema.
Dk. Gwajima aliweka wazi kwamba serikali haitapenda kutumia nguvu wakati wa kusherehekea sikukuu za mwisho wa mwaka kwa kuanza kutoa makatazo mbalimbali.
MIKOA VINARA WA CHANJO
Aidha, waziri huyo aliitaja mikoa mitano inayofanya vizuri katika mapambano dhidi ya Uviko-19, ikiwemo kuhamasisha wananchi kuchanja ni Ruvuma, Mwanza, Dodoma, Kagera na Mara.
Aliitaja mikoa inayofanya vibaya ni Manyara, Njombe, Singida, Iringa na Songwe na kuonya kwamba iwapo hakuna sababu za matokeo hayo mabaya, atazitaarifu mamlaka za uteuzi wa wakuu hao wa mikoa.
Dk. Gwajima alifafanua kwamba, mikoa yote iliyobaki inafanya juhudi za mapambano kiasi na kusisitiza kwamba ni muhimu mikoa yote iongeze bidii kuhakikisha inakuwa katika nafasi nzuri ya kuchanja watu.
Waziri Gwajima alitoa wito kwa wakuu wa mikoa kusimamia na kuratibu kwa kasi mpya mapambano dhidi ya corona, waweke mipango na kufanya tathmini kila baada ya miezi mitatu huku wakikumbuka kwamba wamepewa nafasi hizo kumuwakilisha Rais.
Alitaka watu maarufu watumike kuhamasisha mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Dk. Gwajima alisema pamoja na uwepo wa ongezeko la ugonjwa huo, lakini serikali imekuwa ikihamasisha hatua za tahadhari, ikiwemo kuchanja ili kudhibiti kuenea kwa maambukizi.
Pamoja na juhudi hizo, alisema kumekuwepo na wananchi katika baadhi ya mikoa, jamii na halmashauri wanaochukulia jambo hilo bila uzito na hivyo kuchangia kuongezeka kwa maambukizi.
MWENENDO WA CORONA
Alibainisha mwenendo wa corona Tanzania hadi Desemba 18 mwaka huu, unaonyesha takriban watu 28,214 wamebainika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo, huku 700 wakipoteza maisha.
“Hizo ni taarifa tulizozipata pekee kuna ambao wameambukizwa na kupona bila kupata taarifa na wengine wameugua nyumbanmi na kufariki dunia bila serikali kufahamu,” alisema.
Alifafanua kwamba, hadi sasa asilimia 50 ya chanjo imetumika huku jumla ya Watanzania waliochanjwa wakiwa ni asilimia 2.21, na kuagiza juhudi zaidi zifanywe ili kufikia lengo la kuchanja asilimia 60 ya wananchi.
Waziri Gwajima alibainisha kwamba, mwenendo wa takwimu za sasa ni kwamba kati ya wagonjwa 10 wenye maambukizi ya corona, nane ni wasiochanjwa huku wawili pekee ndiyo waliopata chanjo na hawasumbuliwi zaidi.
Dk. Gwajima alisema kati ya wagonjwa 10 wanaofariki kwa ugonjwa huo saba ni wale wasiopatiwa chanjo huku watatu ndiyo waliochanjwa na kuongeza: “Tena huwa na magonjwa mengine yanayoathiri kinga ya afya zao ukiwemo ugonjwa wa kisukari.”
Aliongeza, “Kwa maana hiyo hakuna ubishi kuwa kuna faida kubwa za kuchanja, tunahitaji kuongeza kasi ya mapambano, ipo mikoa inayofanya vizuri, inayofanya vizuri kiasi na mingine lazima tusukumane,” alisema.
Aliagiza kuongezwa kwa vituo vya huduma za chanjo kufikia 700, halmashauri kuchanja watu 500 kwa siku na 4,000 kwa mikoa kutegemea na ukubwa wake.
Aliweka wazi dhana ya mawimbi ya ugonjwa huo, akisema iwapo ugonjwa utasumbua na kudumu kwa muda wa siku 21 bila kupungua na sababu nyingine za kisayansi, wanasayansi wanaita hali hiyo kuwa ni wimbi jipya.
Dk. Gwajima alisema kwa Tanzania wataalamu wanafuatilia mwenendo wa takwimu zinazowasilishwa na taarifa ya serikali itatolewa rasmi, na kuwakemea wachache wanaoamua kutangaza mambo ambayo serikali haijatamka rasmi.
PROFESA MAKUBI
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, alisema serikali imetekeleza juhudi mbalimbali katika kukabiliana na janga hilo, ikiwemo kupokea chanjo ambapo hadi sasa dozi milioni 4.4, zimeingia na Watanzania milioni 2.1 wameshachanja .
Alisema mpango huo utawezesha kuchanja watu 80,000 hadi 100,000 kwa siku ambapo kila mkoa utatakiwa kuchanja watu 4,000 Hadi 5,000 kwa siku, ndani ya miaka miwili ili kufikia asilimia 60 ya watu waliochanja.
Katibu Mkuu Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Profesa Rizik Shemdoe, alisema walisimamia na kutekeleza mapambano dhidi ya ugonjwa huo awamu ya kwanza kwa mafanikio.
Alisema serikali inaendelea kufanya kazi kwa kushirikiana na viongozi wa kimila na kidini kupata mbinu za kuhamasisha wananchi kuchanja.
Profesa Rizik alisisitiza kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka ni muhimu kushirikiana ili kuwa na namna bora ya kuwafikia wananchi na kuwalinda, hasa wazee vijijini wasiathirike.
MONGELLA
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella, alisema kumekuwa na mafanikio ya mapambano dhidi ya ugonjwa huo kutokana na uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, ambao umewapa nguvu wananchi.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima, alisema katika mkoa wake wamefanya tathmini ya kuangalia nini wamefanya katika awamu ya kwanza na nini, wanapaswa kufanya katika awamu ya pili na mkakati wake ni kuwafikia wananchi wote wasiochanja.
LILIAN JOEL, ARUSHA Na JUMA ISSIHAKA, Dar





























