WAKULIMA wa ngano nchini, wamehimizwa kuzingatia kanuni bora za kilimo ili kupata matokeo mazuri ikiwemo idadi kubwa ya mavuno.
Akizungumza jana, Ofisa Kilimo Msaidizi wa Kata ya Monduli Juu, Roy Mruma, alisema msimu uliopita licha ya kukosa mvua za kutosha, lakini wakulima walipata mavuno mazuri kutokana na ubora wa mbegu.
“Mbegu ya S Select ni nzuri kwa sababu wapo baadhi ya wakulima hawakuweka mbolea, lakini walipata mpaka magunia 11 kwa ekari moja, hivyo kama wangeweka mbolea wangepata hadi gunia 17 mpaka 18 kwa ekari moja,” alisema Mruma.
Mruma aliwataka wakulima wa Monduli kuanzia mwezi ujao kuandaa mashamba na kati ya Februari na Machi mwanzoni waanze kupanda mazao shambani.
“Miaka ya nyuma wakulima wa Monduli walijikita katika kilimo cha shayiri kwa kuwa ngano haikuwa na soko, msimu uliopita wakulima wamelima ngano ya chakula baada ya serikali kupitia CPB kufufua zao hili na kuanzisha kilimo cha mkataba,” alisema Mruma.
Mkulima kutoka Kijiji cha Lendikinyo, Kata ya Sepeku Monduli, Daniel Ole Laizer, alisema mbegu ya S Select imempa mavuno mengi, katika ekari moja alipanda kilo 65 za mbegu na alivuna magunia 18 ya kilo 100 kwa kila moja.
“Ngano ya S Select ni nzuri kwa uzalishaji inatoa matawi mengi katika shamba, niliweka mbolea ikatoa matawi 10 mpaka 12 kwa mche mmoja. Nikaona mavuno yamekuwa mazuri japo nilikuwa nimechelewa kidogo,” alisema.
Mkulima wa Karatu, Daniel Pareso alisema siri ya kupata mavuno mengi ni maandalizi ya mapema na amejipanga kupanda ngano Machi akiwa na matumaini ya kuvuna vizuri.
“Mwaka huu nilipanda mbegu ya ngano ya S Select, imenipa manufaa kwa sababu katika magunia 90 nimepata tani 11 ilikuwa na uzito wa juu, ekari moja nilipata gunia 12,” alisema Pareso.
Na Gift Mongi, Arusha