TUME ya Utumishi wa Walimu Tanzania (TSC), imeipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kufanikisha kupandisha madaraja na kulipa viwango vipya vya mishahara kwa walimu 146,000.
Hayo yameelezwa jijini Dodoma na Mwenyekiti wa TSC, Profesa Willy Komba, wakati akizungumza na waandishi habari kuhusu masuala ya maadili kwa walimu nchini.
Amesema tangu Rais Samia aingie madarakani sekta ya elimu imekuwa ya neema tofauti na vipindi vingine vilivyopita.
Profesa Komba ameongeza kuwa mwaka huu serikali imepandisha madaraja na kulipa viwango vipya vya mishahara ambapo huko nyuma halikufanyika.
“Tume inampongeza Rais Samia na serikali yake kwa kuendeleza juhudi za kuboresha miundombinu ya elimu nchini hususan kupitia fedha ya Uviko-19 zilizotolewa kwa ajili ya kuboresha miundombinu ikiwemo ujenzi wa madarasa,” ameeleza.
Amesema walimu wameendelea kutekeleza majukumu yao kikamilifu kwa kupandisha viwango vya ufaulu kwa shule za msingi na sekondari, licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali ikiwemo utovu wa nidhamu kwa baadhi ya walimu.
Kuhusu vitendo hivyo, mwenyekiti huyo amesema walimu 1,795 walichukuliwa hatua kwa kushitakiwa kujihusisha katika uhusiano wa kimapenzi na wanafunzi pamoja na makosa ya ukaidi.
Profesa Komba amesema kosa la utoro ililiongoza yakifuatiwa na kosa la kughushi vyeti ambapo walimu 461 walishitakiwa.
Amesema kutokana na makosa hayo zipo hatua mbalimbali ambazo zilichukuliwa dhidi ya wahusika kulingana na makosa yao ambapo asilimia 57.1 walifukuzwa kazi huku asilimia 8.5 walipewa kalipio.
“Asilimia 8.5 walishushwa daraja, asilimia 7.6 walishushwa vyeo, asilimia 7.7 walishushwa mshahara huku asilimia 16.8 walipewa onyo,” amefafanua.
Ameeleza kuwa katika kipindi hicho wapo watumishi walioshitakiwa na baada ya kutathimini mashauri yao kwa kuzingatia kanuni, sheria na taratibu waligundua hawakuwa na hatia.
Aidha, Mwenyekiti huyo ametoa wito kwa walimu kuhakikisha wanajua wajibu unaosimamia utumishi wao.
Na Happiness Mtweve, Dodoma



























