SERIKALI ya Tanzania na Burundi zimetiliana saini za awali za makubaliano ya pamoja ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Uvinza, Tanzania hadi Gitega, Burundi yenye urefu wa kilomita 282.
Makubaliano hayo yalitiwa saini mjini Kigoma na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa kwa niaba ya serikali ya Tanzania na Waziri wa Miundombinu, Ujenzi na Makazi, Dk. Deogratius Nsanganiyumwami na Waziri wa Fedha, Bajeti na Mipango ya Uchumi, Dk. Domitien Ndihokubwayo, kwa niaba ya serikali ya Burundi.
Akizungumza baada ya kutia saini hizo, Dk. Mwigulu, alisema serikali za Tanzania na Burundi zimeanza kuangalia maeneo ambayo watapata fedha za kutekeleza mradi huo.
“Mimi na Waziri wa Fedha wa Burundi tunaanza kuangalia maeneo ambayo tunadhani tunaweza kupata fedha kwa utekelezaji wa mradi huu, tunawaambia Watanzania, Warundi na maeneo mengine yatakayonufaika na reli hii kiuchumi kuwa fedha zitapatikana,” alisema.
Alisema Tanzania imekuwa na uzoefu wa kupata fedha za kutekeleza miradi mikubwa ya aina hiyo kama inayoendelea kwa kipande cha Dar es Salaam- Morogoro-Morogoro – Makutopora.
Dk. Mwigulu alisisitiza gharama za mradi huo zitatolewa baada ya kukamilika kwa taarifa za kihandisi lakini inakadiriwa kuwa hazitazidi dola za Marekani milioni 900.
Waziri huyo aliwapongeza Rais wa Tanzania na Burundi kwa kuona umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kwamba, utekelezaji wa mradi huo utafungua fursa za kibiashara siyo tu katika nchi hizo mbili, bali na nchi nyingine zinazopakana nazo.
Naye, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Mbarawa, alisema reli hiyo itajengwa kwa kushirikiana na Burundi, ambapo utekelezaji wake unatarajiwa kuanza hivi karibuni na inakadiriwa kuwa itakuwa inatumia treni za kisasa zenye mwendokasi wa kilometa 160 kwa saa.
Alisema kwa upande wa Tanzania ujenzi wa reli utahusisha kuunganisha kipande cha Uvinza Malagarasi chenye urefu wa kilomita 156, ambapo Burundi wataanzia Malagarasi hadi Musongati – Gitega chenye urefu wa kilomita 126.
“Mradi huu ni muhimu kwa nchi yetu, Burundi na pia Congo (Jamhuri ya Kidemokrasi) ambao hutumia Bandari ya Dar es Salaam kusafirisha mizigo, hivyo kukamilika kwa reli kutarahisisha usafirishaji wa mizigo kwenda katika nchi hizo,” alisema.
Kwa upande wa Burundi, Mawaziri wake Dk. Nsanganiyumwami na Dk. Ndihokubwayo, walisema Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na Rais wa Burundi, Jenerali Evariste Ndayishimiye, walikubaliana ushirikiano kati ya nchi hizo ujikite pia katika masuala ya kiuchumi, hivyo utekelezaji wa mradi huo ni hatua muhimu katika kuzifungua nchi hizo kiuchumi.
Walisema reli hiyo itasaidia kusafirisha takribani tani zaidi ya milioni moja na madini zaidi ya tani milioni tatu kutoka Burundi kupitia reli hiyo na itapunguza gharama za usafirishaji na kuchochea ukuaji wa viwanda, kilimo na uchumi kwa ujumla.
Na Mwandishi Wetu



























