POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, inawashikiliwa watu wawili kwa tuhuma za kula njama na kumuua Barke Rashid (30), mkazi wa Utete, wilayani Ilala, Dar es Salaam, huku ikisema mhusika wa kitendo hicho aliahidiwa kulipwa sh. milioni 1.7.
Tukio hilo lilitokea Januari mosi, mwaka huu, katika nyumba ya kulala wageni inayojulikana kwa jina la Maridadi, iliyoko eneo la Tabata Segerea, jijini humo.
Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Jumanne Muliro, amethibitisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao alipozungumza na waandishi wa habari na kuwataja kuwa ni Kassim Said Abdallah ‘Bounser’ (34) na Charles Geogory ‘White’.
“Watuhumiwa hao wawili tumewakamata na tunawashikilia kwa mahojiano ya kina,”alisema.
Alidai Januari mosi, mwaka huu, mtuhumiwa Abdallah alimtongoza Barke na kuanzisha uhusiano wa kimapenzi, baada ya makubaliano yao walikwenda kulala nyumba ya kulala wageni ya Maridadi.
Akifafanua tukio hilo, Kamanda Muliro alisema mtuhumiwa huyo alitumwa kufanya mauaji hayo, baada ya kupanga njama na Geogory ambaye alikuwa ni mpenzi wa marehemu ambapo walikubaliana amuue halafu atamlipa sh.milioni 1.7.
Kamanda Muliro alisema uchunguzi wa awali umebaini chanzo cha mauji hayo ni wivu wa mapenzi ambapo mtuhumiwa Geogory alidai marehemu alikuwa anamgharamia, lakini alikuwa ana uhusiano na wanaume wengine.
“Mtuhumiwa Abdallah alikodiwa na Geogory kwa malipo ya sh. milioni 1.7 ili ‘amtongoze’ na baadaye amuue mwanamke huyo kwa madai kuwa, alikuwa anamgharamia sana na kumpangishia nyumba, lakini alikuwa na wanaume wengine,”alifafanua.
Katika tukio lingine, Kamanda Muliro alisema wanawashikilia watu sita kwa tuhuma za wizi wa vitabu vya Taasisi ya Elimu Tanzania (TET).
Alisema tukio hilo lilitokea Januari 23, mwaka huu, eneo la Mabibo External Wilaya ya Ubungo, Dar es Salaam na kwamba vitabu hivyo vilikuwa katika viroba 19 ambavyo vilipakiwa katika magari yenye namba za usajili T718 DXW aina ya Pro Box na T931 DNG aina ya Noah.
Kamanda Muliro alisema watuhumiwa hao wanahojiwa kwa kina na watafikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo.
Na IRENE MWASOMOLA



























