JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limethibitisha vifo vya watu wawili na wengine 10 kujeruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea eneo la Kimara Suka, Jijini Dar es Salaam.
Waliofariki wametajwa kuwa ni Amiri Shaabani (15), Mwanafunzi wa Kidato cha Pili, Shule ya Sekondari Mugabe, Issa Hassan (26) huku majeruhi wote 10 ni wakazi wa Kimara Suka.
Akizungumza baada ya kutokea tukio hilo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, alisema ajali hiyo ilitokea Januari 28, 2022, saa 12:15 asubuhi, ilihusisha gari lenye namba za usajili T.814 DGA aina Scania lori ikiwa na Trailer lenye namba T605 CHR.
“Chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa gari T.814 DGA aina ya Scania Lori, kuendesha bila ya kufuata alama za watembea kwa miguu,” alisema.
Pia, Kamanda Muliro alisema gari hilo lilikuwa likiendeshwa na dereva aitwaye Paul Muhagama (37) wakati akitokea Mbezi kwenda Kimara, aliyagonga kwa ubavuni magari mawili, bajaji moja na watembea kwa miguu waliokuwa wanavuka upande wao.
Aidha, Kamanda Muliro alisema miili ya marehemu, imehifadhiwa katika Hosptali ya Mloganzila, dereva wa gari hilo, amekamatwa kwa hatua zaidi za kisheria.
Kamamda Muliro, aliwataja majeruhi wa ajali hiyo kuwa ni Asha Ramadhani (43), Peris John (46), Tuli Ambwene, Maria Linda (15), Ena Gadau (46), Mary Modest (45), Zulfa Hassan (44), Manfred Mtitu (63), Magreth Alex (18) na Amanda Luembu (12).
Pia, Kamanda Muliro alitoa wito kwa waendesha vyombo vya moto, kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani ili kuepuka ajali.
Na IRENE MWASOMOLA



















