HATIMAYE majaribio rasmi ya daraja la Selander (Tanzanite), Dar es Salaam, yameanza ambapo vimeshuhudiwa vyombo mbalimbali vya usafiri vikilitumia kutoka na kwenda katikati ya Jiji hilo.
Pia, imeshuhudiwa watembea kwa miguu, waendesha baiskeli wakipita kwenda katika shughuli zao mbalimbali.
Mbali na vyombo hivyo vya usafiri, daraja hilo lilifurika vijana waliopita huku na kule wakikimbia mchakamchaka huku zikipigwa ngoma kusherehekea kuanza kupita bila ya malipo.
Shughuli hizo zilianza saa mbili asubuhi, zikiwahusisha vijana wa jiji hilo, waliofanya matembezi na wengine wa bodaboda waliopita huku wakipiga honi kuashiria furaha ya kutumiwa kwa daraja hilo.
Vijana waliokuwepo katika eneo hilo, walibeba bendera za Tanzania na mabango yaliyosomeka ‘Miaka 45, mabadiliko tumeyaona’, ‘Na bado kazi inaendelea’ na ‘Miaka 45 ya CCM Dar es Salaam kama Dubai’.
Kwa mujibu wa baadhi ya vijana waliokuwepo katika hafla hiyo, daraja hilo litasaidia kurahisisha usafiri kwa watumiaji wa barabara hiyo.
Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Kinondoni, Sangu Joseph, amesema kabla ya daraja hilo, wakazi wa maeneo ya Masaki, walitumia muda mrefu kwenda na kutoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
Ameeleza kuwa, hali hiyo ilitokana na msongamano wa magari katika barabara ya Ali Hassan Mwinyi, ambayo kimsingi ilielemewa.
Ameongeza kwa kutambua hilo, serikali iliona umuhimu wa kuwarahisishia wananchi usafiri kwa kujenga daraja hilo.
“Ilikuwa kama ndoto hakuna aliyekuwa na uhakika kwamba, huu mradi ungefikia hapa. Leo (jana) hii tunapita hapa tunashukuru sana na huu ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM hivyo tunajivunia ukizingatia Chama kinatimiza miaka 45,” amesema.
Moses Simon, mkazi wa Masaki ameyepita katika daraja hilo, alisema kwamba, serikali imethibitisha haiongei tu, bali inafanya kile inachokisema.
Ameongeza hilo pekee limempa imani kwa viongozi wa Serikali akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye alidhamiri kuukamilisha mradi bila kulegalega.
“Juzi, kabla ya daraja hilo, nilitoka kazini Posta hadi nyumbani Masaki, nimetumia masaa matatu, wakati ni safari ya dakika 30 hadi 45, leo tunapita hapa ni mkeka tu kaka,” amesema.
Mariam Kizungule ambaye ni dereva wa bodaboda katika kituo cha Aga Khan, amesema daraja hilo litakuwa msingi wa kuwaongezea kipato kwa kuwa, watafanya safari nyingi ikilinganishwa na awali, ambapo walilazimika kuchelewa kutokana na msongamano wa magari.
“Ilivyokuwa ukipata abiria wa Masaki anayepita pale Selander zamani unafikiria, pamoja na kwamba sisi huwa tunapenya penya, lakini wakati mwingine gari zilisongamana kiasi kwamba, pikipiki haipati pa kupita,” alibainisha.
Daraja hilo jipya la Salender lina urefu wa kilomita 1.03 na hadi kukamilika kwake limegharimu sh. bilioni 243, ikiwa ni fedha kutoka Serikali ya Korea na mchango wa serikali ya Tanzania.
NA JUMA ISSIHAKA



























