WAKATI timu za taifa za Senegal na Burkina Faso zikichuana leo usiku katika nusu fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), wadau wa soka nchini wamesema mechi hiyo itatawaliwa na kasi.
Senegal itavaana na Burkina Faso katika kipute kitakachopigwa leo saa 4:00 usiku katika Uwanja wa Ahmadou Ahidjo, Yaounde nchini Cameroon, katika nusu fainali ya kwanza ya AFCON inayoendelea nchini humo.
Kesho, mechi ya pili itazikutanisha Misri dhidi ya mwenyeji Cameroon.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam, Kocha wa Ruvu Shooting, Charles Mkwasa, amesema mchezo huo utakuwa na ushindani mkubwa baada ya timu hizo kuonyesha kandanda safi katika hatua za awali.
Mkwasa, mchezaji wa zamani wa Yanga na Kocha wa timu hiyo katika vipindi tofauti, amesema kabla ya mechi Senegal inaweza kupewa nafasi kubwa ya kushinda, lakini uwanjani timu zote zina nafasi kutokana na ubora wa wachezaji wake.
“Naweza kuipa nafasi Senegal lakini huenda mambo yakabadilika ndani ya dakika 90 hivyo timu itakayojiandaa na kutumia nafasi ndiyo itakayopata ushindi,” alisema Mkwasa.
Ameongeza kuwa, mechi hiyo inaweza kutawaliwa na soka la kasi pamoja na matumizi ya nguvu kutokana na aina ya uchezaji wa timu hizo.
Mchezaji wa zamani wa Yanga, Ally Mayay, amesema mechi hiyo haitabiriki na anatarajia kuona vuta nikuvute katika muda wote wa mchezo.
Amesema Senegal inacheza soka la malengo na nguvu sawa na Burkina Faso ambayo inatumia zaidi kasi na kushambulia kwa kushitukiza ili kupata mabao.
Senegal ilitinga nusu fainali baada ya kuiondoa Guinea ya Ikweta kwa kuifunga mabao 3-1 wakati Burkina Faso iliushangaza ulimwengu wa soka kwa kuifunga Tunisia bao 1-0.
Licha ya mechi hiyo, mechi nyingine itakuwa kati ya Misri dhidi ya wenyeji Cameroon itakayochezwa kesho saa 4:00 usiku katika Uwanja wa Olembe.
Misri ilitinga nusu fainali baada ya kuiondoa Morocco kwa ushindi wa mabao 2-1 wakati Cameroon ikiitoa Gambia kwa mabao 2-0.
Na ABDUL DUNIA