WAKATI serikali ikitafuta suluhisho ya matukio ya mauaji nchini, watu ambao hawajafahamika wamemuua kikatili mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Tutuo, wilayani Sikonge, Mkoa wa Tabora, Maria Kazungu (13) na kumnyofoa viungo vya siri.
Kwa mujibu wa baba mzazi wa Maria, Ngassa Kazungu, tukio hilo lilitokea wakati mtoto huyo alipokwenda kisimani kuchota maji baada ya kuagizwa na mama yake.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi Richard Abwao, amethibitisha kuuawa kwa mtoto huyo na kuahidi kuzungumza zaidi na waandishi wa habari baadaye.
Baba mzazi wa Maria alieleza kwa uchungu kuwa mtoto wake alifuata maji awamu ya kwanza na kurejea salama, awamu ya pili ndipo hakurejea nyumbani hadi siku ya pili.
Alieleza baada ya juhudi za kumtafuta, ndipo walipoukuta mwili wake katika moja ya vichaka ukiwa umenyofolewa baadhi ya viungo vya mwili wake na kutobolewa masikio kwa kitu chenye ncha kali.
“Mwananchi mwenzenu nimepata pigo ambalo sitalisahau katika maisha yangu kwani mtoto wangu Maria ameuawa kikatili sana mimi niliamua kumsomesha mwanangu ili siku aje kunisaidia lakini wameamua kukatisha maisha yake, naumia sana,’’ alisema huku akibubujikwa machozi.
Kazungu alisema kutokana na tukio hilo ni vyema vyombo vya ulinzi na usalama vikafuatilia kwa kina kuwabaini wahusika wa tukio hilo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya hiyo, John Palingo, alisema amesikia kuhusu tukio hilo lakini hana taarifa zaidi kutokana na kuwa Dar es Salaam kwa matibabu ya maradhi yanayomsumbua.
“Ni kweli kuna tukio hilo mimi nimepewa taarifa lakini nipo Dar es Salaam kwa matibabu hivyo unaweza kwenda kwa OCD hapo Sikonge,” alieleza kwa ufupi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ulula, Masele Charles, alikiri kuuawa kwa mwanafunzi huyo na kusisitiza ataanzisha ulinzi shirikishi ili kukabiliana na matukio hayo.
Diwani wa kata hiyo, Rashidi Magope, alisema huyo ni mwanafunzi wa pili kuuawa baada ya mwaka jana kutokea tukio kama hilo.
Aliongeza kuwa mauaji hayo yanaleta taswira mbaya katika kata yake na kuwataka wanaohusika kuacha mara moja kujihusisha na vitendo hivyo, huku akilitaka jeshi la polisi kufanya uchunguzi wa kina.
Na Jumbe Ismailly, Sikonge



























