MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, imemwachia huru kwa masharti mfanyabiashara Steven Aloyce (29) maarufu Masaka, baada ya kukiri kosa la kuua bila kukusudia kwa sababu ya sh. 6,000.
Aloyce ambaye alikiri kutenda kosa hilo, eneo la Vingunguti Machinjioni, Dar es Salaam, ameachiwa kwa masharti ya kutofanya kosa la jinai ndani ya mwaka mmoja, baada ya kukiri kumuua bila ya kukusudia Kijuba Mwangu kwa kumchoma kisu eneo la kifuani na mgongoni na kusababisha kifo.
Akisoma hukumu hiyo iliyokuwa ikitolewa kwa njia ya mtandao huku mshitakiwa akiwa mahabusu katika Gereza la Keko, Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Sheria, Jaji Leila Mgonya alisema kutokana na mshitakiwa kukiri kosa la kuua bila kukusudia, anamwachia huru kwa masharti ya kutofanya kosa ndani ya kipindi hicho.
“Mshitakiwa ninamwachia huru kwa masharti ya kutofanya kosa ndani ya mwaka mmoja na ukizingatia amekiri mwenyewe na tayari ameshakaa gerezani kwa kipindi cha miaka mitano bila shaka atakuwa amejifunza,” alisema.
Masaka anadaiwa Oktoba 16, 2017, maeneo ya Vingunguti Machinjioni alimuua bila kukusudia Kijuba Mwangu maarufu Tall.
Awali, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Janeth Magoho akishirikiana na Wakili wa Serikali, Daisy Makakala alidai kesi hiyo ilipelekwa kwa kusomewa maelezo ya awali kisha kuanza kusikilizwa.
Hata hivyo, baada ya mshitakiwa huyo kukumbushwa shtaka, alikiri kuua bila kukusudia na mahakama ilimtia hatiani.
Kabla ya kusomewa adhabu, mshitakiwa aliomba mahakama impunguzie adhabu kwa sababu ana familia inayomtegemea na amekaa gerezani kwa miaka mitano na amekiri kosa lake, hivyo anajutia.
Jaji Leila alisema mshitakiwa bado ni kijana ana wajibu wa kufanya kazi, hivyo amezingatia kuwa amekaa gerezani miaka mitano.
“Umekaa kizuizini utakuwa umejifunza hivyo nimekuachia huru kuanzia leo na utakuwa katika uangalizi,” alisema.
Mshitakiwa baada ya kuachiwa huru kwa masharti, alibaki amesimama gerezani akiwa haamini kilichotokea na baada ya muda alidai atakuwa raia mwema katika jamii.
Akimsomea maelezo ya awali, Wakili Janeth alidai mshitakiwa alidondosha sh. 6,000 usiku na kuomba tochi ili kutafuta na wakati anamulika alitokea Kijuba na kuzichukua.
Alidai mshitakiwa alianza kukimbizana na Kijuba ambapo wakati wa purukshani za kumnyang’anya fedha, alimchoma kisu mgongoni na kifuani, hivyo alianguka na kuomba msaada kwa wasamaria wema.
Ilidaiwa kuwa Kijuba alipelekwa Hospitali ya Amana na alipopimwa alibainika tayari amefariki, ndipo mshitakiwa alikamatwa na kufikishwa kituo cha polisi.
Na SYLVIA SEBASTIAN



























