MKUTANO wa 35 wa Wakuu wa Nchi na Serikali umeridhia na kupitisha ombi la Tanzania la kutaka Kiswahili kuwa lugha ya kazi katika Umoja huo.
Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango amewasilisha ombi hilo la lugha ya Kiswahili kuwa miongoni mwa lugha za kazi katika mikutano ya Umoja wa Afrika(UN).
Dk. Mpango ameongeza kuwa Kiswahili ni miongoni mwa lugha za kiafrika zenye wazungumzaji wengi barani Afrika, ambapo takribani watu milioni 100 wanakitumia Kiswahili pamoja na wazungumzaji kutoka nje ya Bara la Afrika.
Kutokana na umuhimu wa lugha hiyo, Dk. Mpango alisema tayari inatumika katika jumuiya hiyo ikiwemo Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) pamoja na kufundishwa kwa lugha hiyo katika nchi nyingi za Afrika Mashuleni.
Alisema tayari Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limetangaza Julai 7 ya kila mwaka kuwa siku ya maadhimisho ya lugha Kiswahili Duniani.
Mkutano huo, pia umeichagua Tanzania kuwa mjumbe wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika (AU)
Pamoja na mambo mengine mkutano huo, wa 35 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja Afrika (AU) nchi wanachama zimelaani vitendo vya uvunjaji katiba uliopelekea mapinduzi ya kijeshi katika mataifa mbalimbali.
Pia, mkutano huo ulijadili vitendo vya ugaidi vinavyoendelea katika mataifa mbalimbali barani Afrika. Umoja wa Afrika(AU) umeasa majadiliano kuendelea katika nchi hizo ili kurejesha utawala wa kiraia na kidemokrasia.
Katika kupambana na Uviko-19, Umoja wa Afrika (AU) umetoa rai kwa nchi kushirikiana katika kukabiliana na janga hilo ikiwemo kuhakikisha chanjo zinapatikana pamoja na kuyaunga mkono mataifa yalioanza jitihada za kuzalisha chanjo hiyo barani Afrika ikiwemo Afrika Kusini, Senegal na Rwanda.
Na Mwandishi Maalumu, Ethiopia



























