POLISI Mkoa wa Katavi wanamshikilia Mkazi wa Nsemulwa ambaye ni mwalimu wa mafunzo ya dini, Joseph Paulo (27) kwa makosa ya kulawiti watoto wanne ambao majina yao yamehifadhiwa.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, ACP Ali Makame Hamad, amesema mtuhumiwa huyo alikuwa akiwarubuni wahanga hao kwa kuwabeba kwenye pikipiki huku akiwaambia wamsindikize kwenda kufanya shughuli zake za kibiashara sehemu mbalimbali.
“Kila baada ya kumaliza vipindi vyao vya masomo ya dini alikuwa akiwachukua watoto kwenda kuwafanyia vitendo vya kikatili kwa kuwalawiti kwa nyakati tofauti,”alieleza.
Alisema tayari mtuhumiwa amekwisha fikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.
Kutokana na tukio hilo, Kamanda Hamad alitoa wito kwa wazazi na wakazi wa Mkoa wa Katavi kuwa makini kwa kufuatilia mienendo ya watoto wao pindi wawapo shuleni hata sehemu nyingine wanazowapeleka kwa ajili ya kujifunza na sio kuacha suala la ulinzi kwa polisi pekee kwani ulinzi unategemea pande zote mbili.
Katika tukio lingine, Kamanda Hamadi alisema wanamshikilia Mkazi wa Ibindi, Beno Martias (68) na Mkazi wa Itenka A, Nova Issaka (45) kwa tuhuma za kukutwa na meno mawili ya tembo katika Tarafa ya Nsimbo, Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi.
Alisema kuwa Februari 10, mwaka huu katika Kijiji cha Itenka A, polisi waliwakamata watuhumiwa hao wakiwa na meno mawili ya tembo ndani ya mfuko wa sandalusi wakiyasafirisha kwa kutumia pikipiki yenye namba za usajili MC.410 BQW aina ya Sanlg.
Kamanda Hamad alisema upelelezi watukio hilo unaendelea ambapo watuhumiwa watafikishwa mahakama pindi upelelezi utakapokamilika.
NA IRINE TEMU, MPANDA



















