WAZIRI wa Afya, Ummy Mwalimu, amekemea matumizi holela ya vidonge vya kuzuia mimba aina ya P2 na kueleza madhara yake ni makubwa yakiwemo kusababisha ongezeko la ugonjwa wa ukimwi, saratani na ugumba.
Ameeleza hayo baada ya kusambaa kwa ujumbe katika mitandao ya kijamii unaosema ‘amka umeze P2’, ambao alisema ni hatari.
Hatua hiyo imefikiwa ikiwa ni miaka miwili baada ya gazeti la UHURU kuchapisha habari ya uchunguzi iliyoeleza namna matumizi holela ya dawa za P2, yalivyoshamiri na athari zake hususan kwa wasichana waliopo shuleni na vyuoni.
Katika makala hiyo, gazeti la UHURU liliandika namna wasichana hao wanavyotumia P2 kama njugu wakiogopa mimba na sio ukimwi, huku wataalamu wa afya wakiwamo wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi (TACADS), wakieleza namna maambukizi mapya yalivyoongezeka kwa vijana na Mfamasia Mkuu wa Serikali, Daud Msasi, akionya matumizi hayo holela ambayo ni hatari kiafya.
Kutokana na ujumbe huo mitandanoni wa ‘amka umeze P2’, Waziri Ummy alikemea matumizi hayo na kueleza kuwa unaweza kuonekana ni utani, lakini huo ndiyo ukweli hususan kwa baadhi ya watoto wa kike walio shuleni.
Alisema vidonge vya P2 hutumika kuzuia mimba zisizotarajiwa mathalani kutokana na kubakwa, kondomu kupasuka na kwa waliokosea hesabu za siku zao za hedhi, hivyo kujikuta ‘wamefanya yao’ lengo likiwa ni kuepuka kutoa mimba (abortion) au kuzaa watoto wasiowatarajia.
“Hivyo kama serikali tusingependa kuziwekea vikwazo dawa hizi, tunatamani upatikanaji wake usiwe na changamoto, yaani ziwe zinapatikana haraka na kwa kila mwenye uhitaji aliyepata dharura,” alisema.
Waziri Ummy, aliongeza kuwa anatambua kuna upotoshaji wa dawa hizo hususan kwa watoto wa shule, ambao kwa sasa inaonekana wanaogopa zaidi mimba kuliko ukimwi.
“Matumizi holela ya P2 yanaweza kuzalisha matatizo mengine makubwa ya kiafya kwa wasichana au wanawake. Wataalamu wetu wamenihakikishia kuwa matumizi hayo holela na ya mara kwa mara yanaweza kusababisha ugumba na saratani,” alisema.
Alieleza kuwa ni muhimu kuendelea kuliangalia suala hilo kwa mapana, wakati serikali ikiendelea kulijadili na wadau, huku hatua za haraka zikichukuliwa ikiwamo kuongeza kasi ya utoaji elimu ya madhara ya matumizi holela ya dawa hizo.
“Nimeshaelekeza timu yangu kulitekeleza hili haraka, nasi wazazi na walezi tusione aibu kuwaeleza mabinti zetu madhara ya ngono za mapema na kuepuka ngono zisizo salama, kama anaona hayupo tayari kuzaa basi anashauriwa kutumia njia za uzazi wa mpango na siyo P2,” alisema.
Na MARIAM MZIWANDA