MWANAMITINDO na mwigizaji maarufu nchini, Irene Uwoya, amefunguka kuhusu utajiri wake kwamba unatokana na kufanya biashara ndogondogo ambazo zinamuingizia kipato cha kila siku.
Aliyasema hayo wakati akitambulishwa rasmi kuwa balozi wa duka la mavazi ya kike na kiume, lililopo jijini Dar es Salaam kwa muda wa mwaka mmoja.
Irene alisema kuwa watu wamekuwa wakihoji sana kuhusu fedha zake ambazo amekuwa akizipata, lakini alisisitiza kuwa hana kazi yeyote zaidi ya kujishughulisha na biashara ndogondogo ambazo ndiyo zinamuingizia kipato kwa kiasi kikubwa.
Amesema kuwa yeye siku zote huwa hachagui kazi anafanya kazi yeyote ambayo anaona inamuingizia fedha hata iwe sh. 200 na hasubirii kazi ya milioni na ndio hizo zilizomfikisha hapo alipo kwa sasa.
“Nitatenga siku maalumu niweze kuwatambulisha rasmi Watanzania kazi ninayoifanya na watanishangaa sana kwani ni biashara ndogo sana ambazo zinaniingizia kipato cha kunifanya niishi maisha mazuri pamoja na kuitunza familia yangu.
“Sijawahi kusubiria nifanye biashara ya kuniingizia mamilioni kwani niliona nitachelewa zaidi kufikia malengo niliyojiwekea katika maisha yangu,” alisema Uwoya.
Uwoya alisema watu wote ambao wanamshangaa, wajitahidi kufanya kazi kwa bidii ili kuweza kumfikia yeye alipo na wala wasikate tamaa.
Wakati huo huo Uwoya alisema yupo katika mahusiano ambayo ikifika wakati atayaweka wazi na kila mtu atayajua na pia anatarajia kumpata mdogo wake Krish.
“Nadhani kuanzia mwezi wa sita naweza kuwa na mdogo wake Krish kwani ni jambo ambalo nalihitaji sana, lakini kuhusu mahusiano yangu kwa sasa bado sijataka kuyaweka wazi, ila ikifika muda nitamuonyesha mwanaume wangu na kila mmoja atamuona,” alisema Uwoya.
Hata hivyo Uwoya alisema katika suala la bishara kama mtu yeyote anataka kufanya kazi na yeye, anatakiwa kuwa na msimamo na kuongea nini anataka ili kuhakikisha wanakaa chini na kujadili jinsi ya kumsaidia.
Na NASRA KITANA