WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula, amewataka Makamishna Wasaidizi wa Ardhi wa mikoa nchini kuwajibika na kutumia wajibu wao katika kutekeleza mikakati ya Wizara kufikia malengo.
Aidha, amewataka Makamishna hao kuwapangia majukumu maafisa walio chini yao na kufuatilia kazi wanazowapa mara kwa mara.
Dkt. Mabula amesema hayo leo Februari 25, 2022, wakati akifungua kikao kazi cha Menejimenti na Makamishna wa Ardhi Wasaidizi wa mikoa kilichofanyika ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Arusha.
‘’Yapo malalamiko ya lugha zisizofaa kwa wateja, hii haikubaliki fuatilieni hili na kulikemea vikali na kuzingatia misingi na kanuni za utumishi wa umma katika majukumu yenu ya kila siku ’’ amesema Dkt. Mabula.
Aidha, amewataka katika utekelezaji mpango mkakati wa wizara wazingatie vipaumbele vya serikali hususan maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan na ukusanyaji wa maduhuli ya serikali kupitia kodi ya pango la ardhi.
Akigeukia suala la makusanyo ya kodi ya pango la ardhi, Waziri wa Ardhi, amewataka Makamishna wa ardhi Wasaidizi wa mikoa kuwa wabunifu katika njia za kukusanya mapato.
‘’Sula la mtandao kutopatikana muda mwingi linaonekana kuwa kikwazo katika ukusanyaji maduhuli, lifanyieni kazi’’ amesema Dkt Mabula.
Waziri Dkt. Mabula pia amehimiza kuongezwa kwa kasi ya umilikishaji ardhi kwa wananchi na kuwataka Makamishna hao na wakuu wa idara kuweka malengo kwa kila ofisa mwenye taaluma ya ardhi kuandaa hati.
Na Munir Shemweta, WANMM ARUSHA



























