RAIS Samia Suluhu Hassan, ameshuhudia utiaji saini hati za makubaliano ya mikataba 36 yenye thamani ya zaidi ya sh. trilioni 17.3 na kuagiza utekelezaji wa haraka na wa viwango wa mikataba hiyo ili kufika malengo yaliyokusudiwa.
Amesema hayo mjini Dubai wakati wa kongamano la biashara na uwekezaji na utiaji saini wa mikataba 36, iliyohusisha sekta mbalimbali ikiwemo nishati, madini, miundombinu, kilimo na mawasiliano.
Hati 12 kati ya hizo zilizotiwa saini ni baina ya Tanzania na wizara na taasisi za umma na wawekezaji mbalimbali wa sekta za umma na binafsi, ambapo hati moja itahusisha Wizara ya Biashara na Viwanda ya Zanzibar na wawekezaji wanaonuia kushirikiana na kwenye sekta ya utalii.
Vile vile hati za makubaliano zingine 23 zilitiwa saini baina ya kampuni binafsi kutoka Tanzania na kampuni nyine zenye nia ya kushirikiana katika sekta mbalimbali za kiuchumi.
Kupitia mikataba hiyo, idadi ya ajira zinazotawajiwa kupatikana kutokana na makubaliano hayo ni zaidi ya 200,000 katika kipindi cha miaka minne, huku uwekezaji huo ukigharimu sh. trilioni 17.35 za kitanzania.
Sekta zinazotarajiwa kunufaika na makubaliano hayo ni nishati, kilimo, utalii, miundombinu, usafiri na teknolojia. Rais Samia alisema ili kushawishi uwekezaji na kutengeneza bidhaa madhubuti na za kisasa nchi inahitaji elimu bora.
“Serikali ya Falme za Kiarabu (U.A.E) na nchi nyingine zinazoshiriki katika EXPO 2020 Dubai kutoa fursa za masomo kwa wanafunzi kutoka Tanzania kupitia ufadhili na mpango wa ubadilishanaji wanafunzi.
Kwa mujibu wa Rais Samia, Tanzania ni sehemu sahihi ya uwekezaji ambapo aliwakaribisha wawekezaji kuja kuwekeza nchini, kutokana na mazingira mazuri ya kibiashara yaliyopo.
“Tunahitaji kukuza idadi ya wawekezaji kati yetu na nchi za Falme za Kiarabu (U.A.E). Nataka mikataba hii ifanyiwe kazi,” alisema.
Amewakaribisha wawekezaji kutoka U.A.E kuwekeza nchini katika sekta ya mbalimbali ikiwemo utalii, madini, biashara, viwanda, kilimo, uchumi, miundombinu na kwamba kuna fursa nyingi za uwekezaji nchini Tanzania.
Aidha alisema wafanyabiashara wa Tanzania wapo tayari kufanya kazi na wawekezaji kutoka U.A.E
Rais Samia alitoa shukrani zake za dhati kwa U.A.E kwa mapokezi mazuri aliyoyapata yeye na ujumbe wake, wakimwemo mawaziri, makatibu wakuu, wakuu wa taasisi, wawakilishi sekta binafsi, benki, wakuu za taasisi zikiwemo binafsi na umma..
Pia, alipongeza ushiriki wa mawaziri wenye dhamana ya masuala ya uwekezaji na biashara kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar, Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TANTRADE), Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Ubalozi wa A.U.E katika kongamano hilo muhimu la kibiashara.
Amewapongeza pia wadhamini wa kongamano hilo ambao ni Benki ya CRDB, Mamlaka ya Bandari (TPA), Benki ya NMB na wadau wengine waliofanikisha kongamano hilo..
Kwa mujibu wa Rais Samia, Tanzania na Zanzibar ni nchi zilizoungana na ina kubwa wa soko la watu milioni 60 na Tanzania ni mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kwamba kwa ukubwa wake katika soko la Afrika Mashariki ni watu milioni 77 na pia ni mwanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).
Amesema Tanzania ni mwanachama wa SADC jumuia yenye wanachama kutoka mataifa 16 yenye ukubwa wa soko la watu zaidi ya milioni 300 na imeridhia mkataba wa kimataifa wa ushirikiano wa kibiashara unaojumuisha nchi 55 kutoka barani Afrika na hivyo kuwekeza Tanzania na kuwawezesha wawekezaji kulifikia soko la watu wapatao bilioni 1.3.
Kwa upande wake, Waziri wa Biashara na Uwekezaji, Dk. Ashanti Kijaji, alisema atahakikisha mikataba yote iliyotiwa saini inakuwa na manufaa kwa nchi.
Dk. Ashanti alisema kutiwa saini kwa mikataba hiyo ni matunda ya ziara za Rais Samia alizofanya hivi karibuni katika nchi za Ufaransa na Ubelgiji.
Juzi, Rais Samia aliwakaribisha wawekezaji kuwekeza Tanzania, akisema ni mahali sahihi kutokana na amani na utulivu uliopo.
Rais Samia aliyasema hayo akiwa wakati akifungua siku rasmi ya Tanzania katika Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa (DUBAI EXPO 2020).
Alisema Tanzania ni mahali sahihi na rafiki kuwekeza na kufanya biashara kutokana na amani na utulivu wa kisiasa uliopo.
“Niwakaribishe wote Tanzania, mazingira yetu ya biashara ni zaidi ya rafiki, njooni Tanzania, tunawasubiri na wakati wowote mtakapofikiri kuhusu uwekezaji na biashara fikirieni kuhusu Tanzania,” aliwakaribisha wawekezaji.
Alisema Tanzania ni nchi yenye watu wakarimu na sura zilizoshamiri tabasamu wakati wote, hivyo ni vyema wakaja kushuhudia.
Na Mwandishi Wetu