MWAKILISHI kutoka Idara ya Jinsia, Wanawake na Watoto Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Sharifa Abeid, amesema sherehe za maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, zinatoa fursa kujitathimini walipofikia katika harakati za kujiletea maendeleo.
Amesema siku hiyo pia inatoa nafasi kwa wanawake kubaini changamoto na kujipanga kwa mwelekeo wa baadaye ili kukuza maendeleo ya wanawake nchini.
Mwakilishi huyo aliyasema hayo, wakati akitoa risala kwa niaba ya wanawake katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, katika viwanja vya Maisara mjini Unguja.
Alisema wanawake wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla wanaungana na wenzao duniani kote kusherehekea siku hiyo, ambayo inawapa fursa ya kujitathimini katika harakati za kujipatia maendeleo na kubaini changamoto zinazokwaza kukuza maendeleo nchini.
Sharifa alieleza Rais Samia ni kiongozi wa mfano wa kuigwa kwa kuwa ni wa kwanza siyo tu kwa Tanzania, bali Afrika Mashariki.
Alieleza wanawake wa Zanzibar wanampongeza kwa dhati Rais wa Samia, ambaye katika kipindi kifupi cha mwaka mmoja cha uongozi wake umeweka historia kubwa Afrika.
“Sisi wanawake tunakupongeza kwa dhati kuiongoza Tanzania kwa kipindi cha mwaka mmoja sasa, uongozi wako umeweka historia kubwa kwa Afrika Mashariki kuwa mwanamke wa kwanza Rais Tanzania, tunajivunia kuona Tanzania kuwa na Rais mwanamke. Wanawake tunaweza,” alisema.
Aidha, alisema wanawake wanampongeza Rais Samia kwa ujasiri alionao kwa kuiongoza serikali kwa umakini na kuweka vipaumbele muhimu ambavyo vimegusa maeneo mbalimbali ya kimaendeleo katika maisha haki na usawa kwa makundi ya jamii.
Alisema vipaumbele hivyo vinatoa fursa kubwa ya kukuza maendeleo na kuwanufaisha wanawake.
“Mheshimiwa Rais umeweza kuongeza nafasi nyingi zaidi kwa wanawake katika nafasi za uongozi, kwa kuzingatia vigezo na sifa stahiki, kwa mfano katika ngazi za mawaziri umeweza kuwateua mawaziri wanawake wanane kati ya mawaziri 23, katika baraza lako la mawaziri ikiwa sawa na asilimia 35,” alisema.
Pia, alisema Rais alifanya uteuzi wa Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, mwanamke akiwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo na kusema juhudi hizo zimeongeza ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi.
Aidha, alisema katika kuimarisha hali ya uchumi na ustawi wa wanawake, Rais Samia Samia ameweka ahadi katika ngazi za kitaifa na kimataifa ya kuhakikisha wanawake wanawezeshwa kiuchumi na kuwawekea mazingira wezeshi ikiwemo upatikanaji wa rasilimali za uzalishaji mali, ardhi, ujuzi, teknolojia, upatikanaji wa mitaji na uhuduma za kijamii.
“Pia, umeunda kamati maalumu ya kitaifa itakayokushauri katika utekelezaji wa ahadi hizo ambazo uliziweka nchini Ufaransa, ikiwa ahadi hizo zitatekelezeka ipasavyo zitaleta mabadiliko makubwa kwa wanawake na Watanzania kwa ujumla,” alieleza.
Pia alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa kuteuwa mawaziri watano sawa na asilimia 31 na kuwapa madaraka katika nafasi mbalimbali za uongozi.
NA MWANDISHI WETU



















