RAIS Samia Suluhu Hassan, amemuagiza Waziri wa Katiba na Sheria, George Simbachawene, kuandaa kanuni zitakazoelekeza namna vyama vya siasa vitakavyofanya mikutano ya hadhara.
Mkuu wa nchi, ametoa maelekezo hayo baada ya kupokea maazimio ya awali kutoka ‘Kikosi Kazi’ alichokiteua kwa ajili ya kufuatilia hoja zilizojitokeza katika mkutano wa wadau wa demokrasia ya vyama vya siasa, uliofanyika jijini Dodoma Desemba 15 hadi 17, mwaka jana.
Katika utekelezaji wa hilo, Rais Samia alitaka wizara hiyo ishirikiane na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na Zanzibar (ZLS).
Aidha, kikosi kazi hicho chenye wajumbe 24, kiliwasilisha maazimio yaliyogawanyika katika makundi matatu ya muda wa utekelezaji.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu iliyotiwa saini na Mkuu wa Idara hiyo, Zuhura Yunus, makundi hayo ni maazimio ya muda mfupi, wa kati na mrefu.
Taarifa hiyo ilisema, azimio la muda mfupi ni uandaaji wa kanuni zitakazoelekeza jinsi ya kufanya mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa.
Baadhi ya maazimio ya muda wa kati ni rushwa na maadili katika uchaguzi, ruzuku, elimu ya uraia, huku masuala yanayohusu uchaguzi na katiba mpya vikiwa ni maazimio ya muda mrefu.
Maazimio hayo yanapokelewa ikiwa ni miezi kadhaa tangu kikosi kazi hicho kianze kazi kwa mujibu wa maelekezo ya Rais Samia.
MWELEKEO
Kuundwa kwa kikosi kazi hicho ni mwelekeo mpya wa mwenendo wa siasa za Tanzania, wenye lengo la kuweka mazingira ya kufanyika kwa siasa zinazolinda maslahi ya nchi na si siasa za uvunjifu wa sheria, kanuni na taratibu.
Katika jopo lililokutana na Rais jana, yumo mwanazuoni maarufu wa Sayansi ya Siasa Profesa Rwekaza Mukanda, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, Rais wa TLS Dk. Edward Hoseah, Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Zitto Kabwe na wajumbe wengine.




























