RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amezitaka taasisi husika kufanya uchunguzi wa kina juu ya ajali ya moto iliyotokea katika Shule ya Sekondari ya Kengeja Ufundi, Kiswani Pemba na kuunguza bweni la wanawake.
Amesema kwa kufanya hivyo, kutasaidia kukabiliana na majanga ya moto yasiendelee kutokea kwa kuwa, yalishawahi kuripotiwa hivi karibuni katika Shule ya Utaani na Madungu kisiwani humo.
Dk. Mwinyi alisema hayo wakati akitoa salamu za pole kwa wanafunzi na walimu wa shule hiyo kufuatia kuungua moto kwa bweni la wanawake.
Katika salamu zake za pole, Dk. Mwinyi alieleza jinsi alivyopokea kwa mshtuko na huzuni kubwa tukio hilo lililotokea jana na kusababisha uharibifu wa jengo hilo, vitanda, vifaa vya kusomea vya wanafunzi na vifaa vyingine vya matumzi ya wanafunzi.
Alisema Serikali itachukua juhudi za makusudi katika kuhakikisha inawawekea mazingira mazuri kwa wakati huu kwa wanafunzi ambapo itahakikisha hali ya bweni hilo linarejea kama ilivyokuwa mwanzo ili waendelee na masomo yao kama kawaida.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Mattar Zahor Massoud, viashiria vya mwanzo vya tukio hilo la moto vinaonyesha, tukio hilo lilitokana na hitilafu ya umeme na hakuna mwanafunzi aliyepata majeraha na wanafunzi wapo salama.
Alisema jengo liliungua na vifaa vyote vya wanafunzi vilivyokuwemo ndani na kwamba, wanaendelea na uchunguzi kuhusu tukio hilo sanjari na kupeleka misaada mbalimbali ili waendelee na masomo.
Na MWANDISHI MAALUMU, Zanzibar



























