RAIS Samia Suluhu Hassan, amewataka mawaziri kuchapa kazi kwa bidi na kutosikiliza maneno ya watu ili kuharakisha maendeleo ya wananchi.
Alisema hayo alipokuwa akihutubia umati mkubwa wa wakazi wa Mkoa wa Tabora waliofurika katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, akiwa katika siku ya mwisho ya ziara yake ya siku tatu mkoani hapa.
Rais Samia alisema serikali imetekeleza na itaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta zote kwa manufaa ya wananchi, hivyo aliwataka mawaziri kusimamia ipasavyo miradi yao huku akiwataka kutoogopa maneno yanayosemwa na watu wasio na nia njema kwa serikali.
Alibainisha kuwa fedha nyingi zimepelekwa katika halmashauri zote kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ili kuboresha huduma za jamii, hivyo alisisitiza viongozi wa mikoa, wilaya na wakurugenzi kusimamia ipasavyo fedha hizo.
Rais Samia alisisitiza kuwa ataendelea kupeleka fedha zaidi katika sekta zote kwa ajili kutekeleza miradi ya maendeleo na kuwahakikishia wananchi kuwa hakuna atakayeachwa nyuma katika suala la maendeleo.
Aliwataka wakuu wa mikoa na wilaya kuhimiza wananchi kuchangamkia fursa zilizopo katika miradi ya ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) na Bomba la Mafuta na mingineo inayotekelezwa katika maeneo yao.
Pia, alizitaka halmashauri zote kuhakikisha fedha za maendeleo zinapopelekwa wawajulishe wananchi na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho ndicho chenye serikali ili wajue kiasi cha fedha kilichopelekwa na matumizi yake.
“Halmashauri zina fursa nyingi za mapato, jipangeni vizuri ili kuongeza makusanyo, mkiwa na mapato mengi mtairahisishia serikali katika utekelezaji miradi mbalimbali ya wananchi ikiwemo huduma za kijamii,”alisema Rais Samia.
Ili kuharakisha maendeleo ya wananchi, alisema wameongeza fedha katika bajeti ya mwaka huu katika sekta zote kwa lengo la kufanikisha mipango yote ya serikali ili kuboresha hudum za jamii.
Kuhusu tozo za mazao ya wakulima, Rais Samia aliagiza wakurugenzi wa halmashauri zote kutowatoza tozo yoyote wakulima wanaosafirisha mazao ambayo hayajazidi tani moja.
Alisema zana za kujifungulia wajawazito zinapaswa kutolewa bure katika vituo vya afya na hospitali huku akibainisha kuwa ni jukumu la MSD kuhakikisha vifaa hivyo vinasambazwa.
Kuhusu vijiji vilivyoachwa kwenye maeneo ya hifadhi, alisema havipaswi kuendelea kuharibu
hifadhi hizo bali wananchi watunze vizuri mazingira yanayowazunguka kwa kujiepusha na uharibifu wa aina yoyote ile.
Alisisitiza kuwa serikali haitasogeza tena mipaka ya hifadhi, hivyo akawataka wakazi wa vijiji husika kutumia vizuri maeneo waliyopewa kwa shughuli za kimaendeleo.
“Nimelekeza maeneo yote ya uhifadhi yatumike vizuri na yatunzwe kwa manufaa ya nchi na vizazi vijavyo, waliopewa dhamana ya kusimamia maeneo hayo wafanye kazi yao ipasavyo,” alisema.
Rais Samia aliipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge kwa kuanzisha kiwanda cha kuchakata mazao ya nyuki kuongeza thamani ya mazao hayo ambapo alishauri kisimamiwe vizuri ili kilete tija kwa wafugaji.
Aidha, alivitaka vikundi vyote vinavyojishughulisha na ufugaji nyuki kuhifadhi vizuri misitu ili shughuli zao ziwe endelevu na kutoleta athari yoyote katika mazingira.
KAULI ZA MAWAZIRI
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, aliwahakikishia wananchi kuwa serikali imetenga bajeti ya kutosha katika sekta hiyo ili kuhakikisha kilimo kinaboreshwa lengo likiwa kumnufaisha mkulima.
Bashe aliongeza kuwa skimu zote za umwagiiaji zitaboreshwa katika mwaka huu wa fedha ili
kuongeza uzalishaji wa mazao mbalimbali ya wakulima, huku akibainisha kuwa mazao yote yatakayozalishwa yatapata soko la uhakika.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, aliwahakikishia wakazi wa Mkoa wa Tabora kuwa barabara zote zilizoainishwa zitaendelea kuboreshwa ikiwemo kujengwa kwa kiwango cha lami.
Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Juma Aweso, alisema serikali ya awamu ya sita inawajali sana wananchi wake ndiyo maana imeleta maji ya Ziwa Victoria katika mkoa huo kwa gharama ya zaidi ya sh. bilioni 600 ili kutatua kero hiyo.
Aliongeza kuwa baada ya kukamilika kwa mradi huo sasa wanajipanga kufikisha maji hayo katika Wilaya za Urambo na Kaliua na maeneo mengine ambayo hayajafikiwa na huduma ya maji safi na salama.
Waziri wa Nishati, Januari Makamba, alitaja sababu ya kukatika kwa umeme mara kwa mara katika maeneo mengi hapa nchini kuwa ni kutokana na uchakavu wa miundombinu na isiyotosheleza.
Makamba aliongeza kuwa mahitaji ya umeme yameongezeka hadi kufikia megawati 1,336 kutokana na sababu za kiuchumi hivyo alibainisha kuwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linahitaji kufanyiwa maboresho makubwa ya kiutendaji.
Na ALLANI KITWE































