IKICHEZA soka la kisasa katika dimba la ugenini, timu ya Taifa ya wasichana wenye umri chini ya miaka 17 ‘Serengeti Girls’, imekaribia kufuzu fainali za Kombe la Dunia baada ya kuifunga Cameroon kwa mabao 4-1.
Tanzania imeibuka na ushindi katika mchezo wa awali wa raundi ya nne uliofanyika Mei 22, 2022, katika Uwanja wa Ahmadou Ahidjo, uliopo Yaounde, Cameroon.
‘Serengeti Girls’, ikionyesha kiwango bora chini ya Kocha Bakari Shime, ilicheza kwa kuelewana tangu dakika ya kwanza na kupachika bao la kuongoza dakika ya tatu kupitia Diana Mnally, aliyeunganisha mpira wa kona iliyochongwa kutoka winga ya kulia.
Dakika ya 26, Mana Lamine, aliiandikia Cameroon bao la kusawazisha, baada ya kuwahadaa mabeki wa Tanzania na kuachia shuti lililozama wavuni.
Baada ya bao hilo, Tanzania ilijipanga na kufanya mashambulizi ya haraka na kufanikiwa kupachika bao la pili dakika ya 29, likiwekwa kimiani na kinara wa mabao Afrika, Clara Luvanga, aliyepiga shuti lililojaa moja kwa moja wavuni.
Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa Tanzania kwenda mapumziko kifua mbele, na kuanza kipindi cha pili kwa kasi ya kutafuta mabao mengine.
Akijihakikishia kutwaa kiatu cha dhahabu, Clara alifunga bao la tatu dakika ya 63, akiunganisha pasi safi aliyosogezewa na kuijaza kambani na kumuacha kipa akigaagaa chini.
Tanzania iliyokuwa na uchu wa mabao, ilifunga bao la nne kupitia Clara aliyekutana uso kwa uso na kipa kabla ya kuutanguliza mpira wavuni.
Cameroon ilijaribu dakika ya 69, 72, 78 na 83, lakini mipira waliyopiga ilitoka nje.
Katika mchezo huo, mwamuzi aliwaonyesha kadi za njano Clara na Joyce Lema kabla ya kocha kumtoa Diana na kuingia Husna Mpanja.
Dakika 90 za mchezo zilitamatika kwa Tanzania kutoka dimbani na shangwe la ushindi mnono.
SOPHIA ASHERY, Cameroon