MJADALA wa Bajeti ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, umezua tafrani ndani ya Bunge baada ya Mbunge wa Mbulu Vijijini (CCM) Flatei Maasai, kuruka sarakasi huku Mbunge wa Ukonga (CCM) Jerry Silaa, akiangua kilio wakati wakichagia mjadala huo bungeni.
Flatei alilazimika kuruka sarakasi juu ya meza kama hatua ya kuonyesha msisitizo kwamba, wizara hiyo imekuwa ikitoa ahadi hewa ya ujenzi wa barabara ya Mbulu – Haydom.
Naye, Silaa aliangua kilio wakati akichangia mjadala huo wa bajeti kwamba kampuni ya Syno Hydro iliyopopewa zabuni kujenga barabara ya mwendokasi kuanzia Kariakoo hadi Gongo la Mboto, jijini Dar es Salaam, imefanya vibaya katika miradi mingine.
Flatei alisema katika bajeti ya mwaka jana ilitolewa ahadi kujengwa barabara hiyo lakini Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, imeonyesha fedha zilizotengwa zimepelekwa kulipa madeni.
Mbunge huyo alieleza kuwa katika kitabu cha bajeti cha mwaka wa fedha 2022/2023, imeonyeshwa kuwa barabara hiyo itajengwa katika kiwango cha lami lakini kwa Kilometa 25.

“Mheshimiwa spika nisaidie ninafanyaje? Nimezungumza nao sana, inatosha. Mipango yote nimefuata utaratibu wote nimefuata inatia uchungu mheshimiwa Spika,” alisisitiza.
JERRY AANGUA KILIO
Naye, Mbunge wa Ukonga, Silaa alimwaga machozi bungeni wakati akieleza kampuni ya Syno Hydro iliyopewa zabuni ya kujenga barabara ya mwendokasi kuanzia Kariakoo hadi Gongo la Mboto, kwamba imevurunda katika miradi mingine.
Akichangia mjadala wa bajeti ya wizara hiyo, Silaa alidai kampuni hiyo imepewa miradi katika sekta mbalimbali ikiwemo maji, lakini imekuwa akichelewesha kukamilisha kazi na malipo ya wafanyakazi.
Alisema katika barabara, imegundulika kuwa umbali wa kilometa 2.5 wa barabara ya mwendokasi kuanzia Gerezani hadi Mbagala, ubovu umebainika.
NA MUSSA YUSUPH, DODOMA



























