WIZARA ya Kilimo, inatarajia kuzalisha miche milioni 20 ya kahawa kisha kuigawa kwa wakulima kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa zao hilo.
Kauli hiyo, ilitolewa Bungeni jijini Dodoma wakati Naibu Waziri wa Kilimo, Antony Mavunde, akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Ghati Chomete.
Mbunge huyo, alihoji kuwa ni lini Serikali itatekeleza mkakati wa kuongeza uzalishaji wa kahawa aina ya arabika.
Akijibu swali hilo, Mavunde alisema moja kati ya mikakati ya kukuza zao la kahawa nchini ni uzalishaji na usambazaji wa miche bora ya kahawa, kuwawezesha wakulima wengi wazalishe kwa tija
“Mwaka huu, tumejipanga kuzalisha miche milioni 20 na kuwafikia wakulima wengi kadri iwezekanavyo, huu ni mkakati wa serikali wa kukuza zao la kahawa kwa kuwafanya wakulima kuzalisha kwa tija,” alieleza.
Awali, Mavunde alisema serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia (WB), imetekeleza Mradi wa Kuongeza Uzalishaji na Tija ya zao la Mpunga (ERPP) katika Mkoa wa Morogoro.
Kauli hiyo aliitoa wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalumu, Aleksia Kamguna, ambapo mbunge huyo alihoji serikali ina mpango gani wa kuboresha kilimo cha mpunga katika Mkoa wa Morogoro.
Akijibu swali hilo, naibu waziri huyo, alisema serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia, imetekeleza mradi wa Kuongeza Uzalishaji na Tija ya zao la Mpunga (ERPP) katika Mkoa wa Morogoro.
Alisema matokeo hayo, yamechagizwa na kuongezeka kwa upatikanaji mbegu bora za mpunga.
Vilevile, alisema ujenzi wa maghala ya kuhifadhia mpunga ulifanyika katika Halmashauri za Wilaya za Mlimba, Ifakara, Kilosa na Mvomero ambapo jumla ya maghala matano, yamejengwa.



























