MKAZI wa Mtaa wa Kebikiri Rebu, Kata ya Turwa, wilayani Tarime, mkoani Mara mwenye umri wa miaka 53, amehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 20, baada ya kupatikana na hatia ya kuzini na binti yake.
Hukumu hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki katika Mahakama ya Wilaya ya Tarime, mbele ya Hakimu Yohana Myombo, baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri ambao haukuacha shaka yoyote.
Mtuhumiwa huyo anadaiwa usiku wa Desemba 21, mwaka jana, alizini na binti yake (jina tunalihifadhi).
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu huyo alisema kutokana na tukio hilo binti huyo alilalamika kwa kutoa taarifa kwa mama na ndugu zake kuhusu kitendo hicho cha ukatili.
“Binti huyo ambaye ni mhanga wa tukio hilo waliongozana na mama na ndugu zake kwenda kutoa taarifa kituo cha Polisi Tarime na kufungua jalada na kupewa fomu ya polisi namba tatu na kufanyiwa uchunguzi hospitali ya wilaya, ambapo iligundulika kufanyiwa kitendo hicho,” alisema.
Alisema wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo, upande wa Jamhuri ulikuwa na mashahidi wanne akiwemo binti huyo, nyaraka za hospitali, mganga aliyemfanyia uchunguzi huku upande wa mshitakiwa akijitetea mwenyewe.
Akijitetea mahakamani hapo, mshitakiwa alidai kesi hiyo ilitengenezwa na ndugu zake ambao wana chuki naye kwa muda mrefu.
Hakimu Myombo alisema kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani hapa na upande wa Jamhuri umethibitisha shtaka dhidi ya mshitakiwa bila ya kuacha shaka yoyote, hivyo anatiwa hatiani kwa kitendo alichokifanya.
“Kutokana na kitendo cha unyama cha kuzini na binti yako, ninakuhukumu kwenda jela miaka 20 ili iwe fundisho kwako na watu wengine wenye tabia kama wewe,” alisema.
Wakati huo huo, Hakimu Myombo alimhukumu Mkazi wa Kijiji cha Kinesi, Tarafa ya Suba, wilayani Rorya, Chacha Kinemo, kutumikia kifungo cha miakamitatu gerezani na kulipa fidia ya sh. milioni mbili, baada ya kukiri kosa la kumwagia petroli kisha kumchoma moto mdogo wake.
Mshitakiwa huyo alidaiwa kumchoma Bina Chacha kwa petroli mikononi kisha kumuwashia moto kwa kutumia kibiriti na kumsababisha ulemavu wa kudumu akidai alimuibia sh. 185,000.
NA SAMSON CHACHA, Tarime



























