KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo, amesema Bajeti Kuu ya Serikali imekidhi mahitaji ya wananchi.
Alisema bajeti hiyo inakwenda kumrahisishia mwananchi maisha, ikiwemo sekta ya elimu baada ya kutolewa malipo ya ada kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita.
Akizungumza jijini Dodoma, baada ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba kumaliza kuwasilisha bejeti hiyo, Chongolo alisema maeneo makubwa yameelekezwa katika kubana matumizi ili kuendana na mazingira ya wakati uliopo.
“Naipongeza serikali kuwasilisha bajeti yenye mwelekeo mzuri na kutekeleza tuliyoahidi kwa wananchi. Bajeti imeangalia mazingira ya kuwarahisishia maisha wananchi wa kawaida, hasa ukizingatia wengi walikuwa wakielekeza nguvu katika kulipa gharama za elimu kwa watoto wao,” alisema Chongolo.
Aidha, alisema nguvu iliyoelekezwa katika kilimo cha umwagiliaji, itasaidia kuimarisha uchumi na kuongezeka pato la taifa.
“Uchumi wa nchi unategemea kilimo, nguvu kubwa iliyowekezwa itapunguza uingizwaji wa bidhaa kutoka nje, tutasafirisha bidhaa na tutongeza pato la nchi, kwa kweli bajeti imejikita katika maeneo muhimu na ndiyo utekelezaji wa Ilani,” alisema.
WABUNGE WAELEZA
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ambaye pia ni Mbunge wa Kilindi (CCM), Omari Kigua, aliipongeza serikali kufuta ada kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita.
“Hii itafanya wanafunzi wengi waendelee na masomo kwani wengi walishindwa kulipa ada, nampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali Watanzania wanyonge,” alisema.
Naye Mbunge wa Hai (CCM), Saashisha Mafuwe, alisema bajeti hiyo inagusa maisha ya uchumi wa mtu mmoja mmoja na inakusudia kuongeza pato la taifa kwa kuwa bajeti ya kilimo imeongezeka kutoka sh. bilioni 294 hadi sh. bilioni 954.
“Viashiria vyote vya kuimarisha kilimo vimewekewa fedha, lakini pia uongezaji thamani mazao ya wakulima na wafugaji vimezingatiwa,” alibainisha.
Mbunge wa Mpanda Mjini (CCM), Sebastian Kapufi, alisema suala la kubana matumizi ni la msingi na amefurahishwa na ongezeko la bajeti ya kilimo inayolenga kuboresha kilimo cha umwagiliaji.
“Mikopo kwa wachimbaji wadogo wa madini, ufunguaji nchi kupitia barabara na uendelezaji wa miradi ya kimkakati kama bwawa la Nyerere na Reli ya Kisasa (SGR),” alisema.
WALIMU WAZUNGUMZA
Mwenyekiti wa Chama Cha Walimu (CWT) Mkoa wa Dar es Salaam, Jastin Runyoro, aliipongeza serikali kwa mabadiliko makubwa yanayotarajiwa kufanyika katika bajeti hiyo mpya, hasa katika upande wa elimu.
Alisema ongezeko la mishahara litasaidia kuleta hamasa kwa walimu kufanya kazi kwa bidii na kuleta matunda katika ufundishaji na matokeo mazuri kwa wanafunzi.
“Suala la kufuta kodi kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita, itasaidia sana vijana hao kufikia ndoto zao na kuongeza wasomi zaidi na kuondoa kasumba ya kushindwa kufikia maono yao kwasababu ya kukosa elimu, hivyo naipongeza serikali kwa kuliona kundi hilo la kaya masikini,” alisema.
Naye Meneja wa shule za Perfect Destiny na Kazaura zilizopo Mkuranga na Temeke, Rodrick Kizito, liipongeza hatua ya serikali kuboresha masilai ya walimu hali itakayoleta matokeo makubwa ya ongezeko la ufaulu.
Alisema suala la serikali kuboresha mitaala na ujenzi wa vyuo vya Tehama na Vyuo Vya Ufundi (VETA), litasaidia kuzalisha vijana wenye ujuzi unaoendana na soko la sasa, badala ya kujifunza nadharia pekee.
KAULI YA BAKITA
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA), Consolatha Mushi, aliipongeza serikali kuendelea kusimamia ukuzaji Kiswahili kwa kasi ndani na nje ya nchi.
WAMACHINGA WAMPONGEZA RAIS
Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Wadogo (machinga) Taifa, Steven Lusinde, alisema serikali ya awamu ya sita inaendelea kutekeleza maagizo ya wananchi hasa katika suala la maendeleo.
Alisema umakini wa serikali hiyo, imetokana na kufanya kazi kwa kutumia Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
Lusinde alisema tayari walishatoa changamoto zao mbele ya Rais Samia kuhusiana na mitaji ya kuendeleza biashara zao na miundombinu yao ya biashara.
Lusinde alisema bajeti iliyosomwa jana bungeni, imekuwa mkombozi kwa wafanyabiashara kwa kutengewa sh. bilioni 45 kwa ajili ya mitaji na miundombinu.
Na WAANDISHI WETU