JOSIAH Ekwabhi Mufungo hatunaye tena katika dunia hii. Mufungo hatunaye tena kwa sababu alifariki juzi usiku mjini Dar es Salaam. Mufungo ni mtu aliyekulia katika tasnia ya habari tangu ujana wake, akiwa na umri wa miaka 20.
Alizaliwa Januari 4, 1953 Majita, Musoma. Mufungo ambaye baada ya kustaafu akiendelea na shughuli zake, alipatwa na ugonjwa wa kiharusi ambao kwa kiwango kikubwa ulitikisa afya yake hadi umauti unamfika.
Mwandishi wa makala hii (Joe Nakajumo), alimkaribisha Mufungo alipojiunga na magazeti ya Chama cha Tanganyika African National Union (TANU), Uhuru na Mzalendo wakati huo yakiwa chini ya Mwananchi Publishing Company Ltd, ofi si zikiwa eneo la viwanda barabara ya Pugu kwa sasa barabara ya Nyerere, umbali wa karibu kilomita tatu kutoka katikati ya jiji ilipo sanamu ya askari wa zamani kwenye makutano ya mitaa ya Samora, Azikiwe na Makunganya.
APATA AJIRA UHURU
Alijiunga na magazeti ya Uhuru na Mzalendo, Oktoba Mosi, 1973, akitokea Idara ya Ushirika katika Wizara ya Kilimo na Maendeleo ya Ushirika.
Mufungo aliajiriwa siku moja na wenzake wakiwemo Hamis Daudi Mkwinda na Kohereth Magessa. Mhariri Mtendaji aliyewaajiri akina Mufungo na wenzake alikuwa Komredi Ferdinand Ruhinda.
Mufungo alianza taaluma ya uandishi akiwa mwandishi wa habari mwanafunzi. Marehemu aliungana na vijana wengine akiwemo mwandishi wa makala hii katika chumba cha habari tukiwa waandishi wanafunzi.
Mwalimu wetu mkubwa aliyetufundisha uandishi wa habari alikuwa Mhariri wa Habari, Kusai Kamisa. Kwa kweli tunamshukuru marehemu Kusai Kamisa kwa sababu alitupika kikamilifu na kutuwekea misingi katika hatua mbalimbali za kutafuta na kuandika habari.
MUFUNGO NA WENZAKE WANOLEWA
Kundi la vijana waandishi wanafunzi katika chumba cha habari cha Uhuruna Mzalendo, wakiwemo, Mufungo, Mkwinda, Magessa, marehemu John Mkamwa, Nakajumo, tulinolewa vizuri na Kamisa. Ye yote kati yetu aliyetumwa kufuatilia habari, halafu anarudi bila habari na kutoa maelezo ya kubabaisha, alihojiwa kikamilifu na Kusai na hata kumrudisha tena alikokuwa ametumwa.
Mufungo aliyezeekea chumba cha habari na kushika nyadhifa mbalimbali hadi ngazi ya juu kabisa ya Mhariri Mtendaji, alistaafu Januari 4, mwaka 2013. Hata hivyo aliendelea kushikilia nafasi ya Mhariri Mtendaji kwa miezi 10 hadi Novemba 4, mwaka huo huo wa 2013 alipoondoka rasmi.
Kunolewa ndani ya chumba cha habari kabla ya kwenda kwenye chuo cha uandishi wa habari kulisaidia sanakupata waandishi wenye upeo mkubwa kitaaluma.
Baada ya kukomazwa ndani ya chumba cha habari, Mufungo alipata mafunzo ya awali ya miaka miwili ya uandishi wa habari katika chuo cha Nyegezi Social Training Centre, Mwanza. Alihitimu Aprili 11, 1975.

Aliporejea chumba cha habari baada ya kufuzu huko Nyegezi, Mufungo aliendelea kuwafunza ndani ya chumba cha habari waandishi wanafunzi. Kutokana na umahiri wake na kwa kuwa aliipenda sana kazi, alisogezwa kutoka dawati la habari na kuwa msanifu.
Mufungo alisogezwa kwenye dawati la usanifu mwaka 1976 kutokana na umakini na utulivu wake katika kupitia habari zilizoandikwa na waandishi.
Vijana waandishi wanafunzi walinufaika sana na utendaji wake kwa mafunzo aliyokuwa akiwapatia. Wakati huo Uhuru na Mzalendo ilikuwa inapokea wanafunzi kutoka Chuo cha Uandishi wa Habari Tanzania (Tanzania School of Journalism (TSJ), ambao pamoja na wahariri wenzake alisaidia kuwakuza kitaaluma.
USANIFU WAMZEESHA
Dawati la usanifu limemzeesha Mufungo kwa sababu alikuwa anapitia habari neno kwa neno, sentensi kwa sentensi, ibara kwa ibara na kubuni vichwa vya habari. Ni mtu aliyekuwa anaingia asubuhi na kuendelea kuchakarika hadi usiku wa saa mbili au saa tatu, gazeti linapopelekwa kuchapwa mtamboni.
Akiwa katika dawati la usanifu, Mufungo hakusita kumwita mwandishi ili afafanue pale ambapo aligundua pana tatizo.

Katika kujiendeleza kitaluma, Mufungo alifi kia ngazi ya kupata shahada ya Masters (MA) katika uandishi wa habari. Aliipata mwaka 1987 katika Chuo cha Cardiff huko United Kingdom, Diploma ya Uandishi wa Habari mwaka 1979 katika chuo cha Berlin Mashariki nchini Ujerumani Mashariki.
Pia alipata fursa ya kufanya ziara za mafunzo katika nchi za Yugoslavia, Urusi, Iraq, Marekani, Uswisi, Uholanzi, Afrika Kusini, Namibia na China.
KAULI ZA ALIOFANYANAO KAZI
Juni, 14, 2022, asubuhi nilipopata taarifa ya kifo cha Mufungo, nilimpigia simu Ndimara Tegambwage mwandishi wa habari mkongwe ambaye sote watatu tulifanya kazi pamoja Uhuru na Mzalendo.
“Je umepata taarifa ya kifo cha Mufungo,” nilimuliza Ndimara naye akanijibu hakuwa na taarifa yoyote. Basi nikamueleza kuwa mwenzetu ametuacha amefariki usiku wa kuamikia Juni 14, 2022.
Ndimara akasema ‘oooh namkumbuka na Suzuki yetu. Wakati tupo Uhuru na Mzalendo Ndimara alikuwa na pikipiki aina ya Suzuki ambapo kwa nyakati fulani alikuwa akimbeba Mufungo.
Nilimpigia Ndimara kumpa taarifa ya kifo kwa sababu juma lililopita nilikutana naye katika barabara ya Uhuru sote tukitembea mimi nikitokea Ilala na mwenzangu akitokea mjini. Aliniuliza vipi Mufungo anaendeleaje, nikamjibu tu kwamba bado anaumwa.
Basi Ndimara akashauri kwamba tutafute siku tuende tukamuone, lakini tusiende peke yetu, ila tuwaombe baadhi ya wafanyakazi wa Uhuru wale aliofanya nao kazi tuende nao pamoja.
Lakini safari hiyo hatukuweza kuifanya hadi mwenzetu umauti unafika. Lakini pia mwaka 1976, Ndimara, Mufungo na Nakajumo tulipelekwa Chuo cha Chama, Kivukoni kwa mafunzo ya itikadi ya miezi mitatu. Baada ya kurudi kazini Uhuru na Mzalendo sisi watatu tulijenga utamaduni wa kuitana “Ndugu Kiongozi.”
Baadhi ya wafanyakazi aliowaacha Uhuru na Mzalendo walimwelezea Mufungo alivyopenda kazi yake. Scolastica Matei alisema;” namkumbuka Mufungo kwa ujasiri wake katika kazi.
Hakuchagua kazi, alisaidia kusoma kurasa za matangazo, akiwa kama mkuu, hakuwa na makuu.”
Rohoida Lwehela alimwelezea Mufungo kuwa alikuwa “mcheshi, mkarimu na mlezi na sio mchoyo wa kufundisha.
Alinifundisha kuandika barua za kiofisi.” Rohoida ni katibu muhtasi. Kwa kweli Mufungo kwa lugha ya siku hizi tunathubutu kusema alikuwa “JEMBE”, Mungu ailaze mahali pema peponi, Amina.
Na JOE NAKAJUMO