MAHAKAMA ya Mkoa wa Wete, imemhukumu mkazi wa Pandani, Ali Sharif Ali (19), kutumikia kifungo cha miaka 20 jela na kulipa fidia sh. 100,000, baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumlawiti mtoto mwenye umri wa miaka 15.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu wa Mahakama ya Mkoa B Wete, Ali Abrahman Ali, alisema mahakama imemtia hatiani kijana huyo, baada ya kuridhika na ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo.
Hakimu Ali amesema ushahidi uliowasilishwa na upande wa Jamhuri umethibitisha shtaka dhidi ya mshitakiwa pasi na kuacha shaka yoyote, hivyo mahakama inampa adhabu ya kutumikia kifungo cha miaka 20 jela na kulipa fidia sh.100,000.
“Tumemtia hatiani mshitakiwa huyo chini ya kifungu 220 cha Sheria ya Mwenendo wa Jinai namba 7 ya mwaka 2018 na kifungu cha 115 (1) cha Sheria ya Adhabu Namba 6 ya mwaka 2018 za Zanzibar,” alisema.
Awali, Wakili wa Serikali, Juma Mussa, aliiomba mahakama itoe adhabu stahiki kama ilivyoelezwa katika sheria, ili iwe fundisho kwa mshtakiwa na wengine wenye tabia kama hiyo.
Kabla ya kusomwa hukumu, mshitakiwa aliiomba mahakama impunguzie adhabu, ombi ambalo lilikataliwa na mahakama.
Mshitakiwa alitenda kosa hilo, Desemba 11, mwaka 2021, saa 1:30 usiku, eneo la Kijuki Pandani, Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, ambapo alimlawiti mtoto menye umri wa miaka 15 (jina tunalihifadhi).
Shauri hilo lilianzwa kusikilizwa kwa mara katika Mahakama ya Mkoa B Wete Januari 13, mwaka jana, ambapo mashahidi sita wa upande wa Jamhuri, akiwemo mtoto walitoa ushahidi.
Na EMMANUEL MOHAMED