SERIKALI imesema hakuna vijiji vya wananchi katika eneo la Loliondo na Simanjiro, ambavyo vimetangazwa kuwa sehemu ya mapori ya akiba, huku wabunge wakikemea vitendo vya baadhi ya wanasiasa na wanaharakati kupotosha umma kuhusu wananchi wa Loliondo kwa kisingizio cha haki za binaadamu.
Imesisitiza eneo lote la ardhi ya Tanzania ni mali ya umma, hivyo maeneo ya mapori tengefu yaliyopandishwa hadhi kuwa mapori ya akiba kwa mujibu wa tangazo lililotolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii, hayahusishi makazi ya watu.
Mjadala huo mkali uliibuka bungeni wakati wabunge wakichangia Hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 baada ya Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka, kudai jamii ya wafugaji inapitia katika taharuki kufuatia uamuzi wa serikali katika eneo la Ngorongoro na kupandisha hadhi baadhi ya mapori tengefu kuwa mapori ya akiba.
Alidai uamuzi huo wa Wizara ya Maliasili na Utalii kupandisha hadhi mapori hayo, unamaanisha Simanjiro itakuwa pori la akiba kwa asilimia 100.
Hata hivyo, alidai uamuzi huo unakinzana na matakwa ya sheria ambayo inaeleza hakuna ardhi ya kijiji itakayogeuzwa pori la akiba.
“Tangazo hilo linataka eneo lote la Simanjiro na eneo lote la Wilaya ya Longido kuwa pori la akiba. Kana kwamba hiyo haitoshi eneo la Ngorongoro lililokuwa Tarafa la Sare, nalo linamegwa kwa sura hii,” mbunge huyo alieleza katika mchango wake.
Wakati Ole Sendeka akiendelea na mchango wake, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Marry Masanja, alisimama kumuomba Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, kumpatia nafasi ya kutoa taarifa kwa mchangiaji.
Naibu waziri huyo alipopewa nafasi alisema taarifa ya Waziri wa Maliasili na Utalii, iligusia maeneo ambayo hayatahusisha vijiji vya wananchi, hivyo maeneo yatakayopandishwa hadhi ni maeneo muhimu ya uhifadhi na hakuna vijiji vya wananchi.
Mara baada ya kutoa taarifa hiyo, Ole Sendeka alikataa kuipokea huku akitaka kutoa ufafanuzi zaidi jambo ambalo lilimlazimu Spika Tulia kumuhoji mbunge huyo kwa lengo la kutaka kupata ufafanuzi kuhusu madai hayo.
“Taarifa ya waziri inasema maeneo yaliyopandishwa hadhi hayana wananchi, mbunge anasema maeneo yana wananchi, upotoshajji upo katika maeneo gani? Hebu waziri tupe ufafanuzi na kama hakuna mwananchi, mchango wa Ole Sendeka nina mazungumzo nao,” aliagiza Dk. Tulia.
Akitoa ufafanuzi zaidi Naibu Waziri Marry alieleza: “Maeneo hayo yalikuwa mapori tengefu yana wawekezaji, tunapoona yana sifa ya kuhifadhiwa tunayapandisha hadhi ili wananchi wasiyasogelee.
“Tumeona haya maeneo yana hadhi na hayana wananchi. Tanzania ardhi ni ya umma, tunawagawa wananchi tunaposema haya maeneo ya kwangu. Asilimia 100 haya maeneo hawapo wananchi,” alisisitiza.
Baada ya kauli hiyo, spika alimtaka Ole Sendeka kusoma vifungu vya sheria vinavyosema mapori tengefu yamefutwa katika maeneo hayo, jambo ambalo mbunge huyo alinukuu baadhi ya vifungu ambavyo spika hakukubaliana navyo.
Kwa sababu hiyo Dk. Tulia alisema: “Maelekezo ya waziri mwenye sekta yanayosema wananchi wa Simanjiro na mapori tengefu wanaondoka, hakuna. Sasa haya maneno ya maeneo wanayokaa wamasai katika wilaya nne wataondoka yametoka wapi?. Waziri amesema maeneo hayo hakuna watu.
“Ukiambiwa unazikosea kanuni zetu kwa sababu umesema jambo ambalo halipo?. Kazi yangu hapa kusimamia kanuni, tukiendelea na mtindo huu mheshimiwa Ole Sendeka mimi nitataka uniletee ushahidi na waziri naye ataleta wa kwake halafu nitafanya maamuzi,” alisema.
Aliongeza: “Nilitaka nikurahisishie kama huna uhakika na hicho unachokisema tuliachie hapo. Kama unao uhakika nitataka uniletee ushahidi na waziri aniletee ushahidi na siyo ushahidi uliousema hapa. Mheshimiwa Ole Sendeka nakupa hiyo nafasi.”
Mara baada ya kupewa nafasi hiyo, Ole Sendeka alifuta maneno yake na kuendelea kuchangia mjadala huo wa bajeti kuu ya serikali.
Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalumu (CHADEMA) Jesca Kishoa, alisema ripoti ya utafiti ya Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) ya mwaka 2020 inaeleza idadi ya watu eneo la Ngorongoro imeongezeka mara tano zaidi ya miaka ya 1970.
Alisema katika eneo hilo idadi ya mifugo imeongezeka kutoka 19,100 hadi 805,000, ambapo mwaka 1970 kila mtu mmoja alikuwa akiishi wastani wa kilomita moja za mraba, lakini mwaka 2019 uwiano ulifikia mtu mmoja akiishi kilomita za mraba 0.084 sawa na watu 11 kukaa katika kilomita moja ya mraba, bila kujumuisha eneo la kuishi wanyama.
“Wanasiasa na wanaharakati waache kupotosha wananchi kupitia kiraka cha haki za binadamu, ninaungana na Rais Samia Suluhu Hassan kulinda urithi wa Tanzania, ninaungana na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika kulinda urithi wa taifa, ninaungana na wananchi kulinda urithi wa taifa,” alisema.
Alisisitiza: “Mkuu wa nchi asirudi nyuma, vizazi na vizazi vitamkumbuka. Tunahitaji keki hiyo ya taifa inufaishe vizazi na vizazi, tuambieni ukweli ni wapi Afrika
Mashariki kilikowahi kufanyika kilichofanyika pale Handeni? Unapelekwa eneo unajengewa nyumba, hospitali, shule na zahanati.
“Kuna taarifa wapo wabunge wanatetea haya kwa maslahi ya mashemeji zao humu. Kusema kuwahamisha ni makosa kwa sababu wameyazoea tunajenga kitu kibaya, endapo wengine wakihamishwa ili kujenga miundombinu watakataa wakisema mbona Ngorongoro walikataa kwa sababu maeneo yao wameyazoea,” alisisitiza.
Mbunge huyo alishauri hatua rafiki zifanyike wakati wa kuwahamisha wananchi katika eneo hilo na kuainisha idadi ya wananchi wanaohitajika kubaki.
Pia, alisema ni muhimu eneo ambalo wananchi hao wanapelekwa wapelekwe madaktari na walimu wa kutosha.
Mbunge wa Mvumi (CCM), Livingstone Lusinde, alisema kwa matendo yasiyokuwa ya kizalendo yanayoendelea, ipo siku huruma ya Rais Samia itaondoka.
Lusinde alisema hakuna katika Tanzania watu waliohama vizuri kama wanaohamishwa kutoka Ngorongoro.
Alisema katika miaka iliyopita wakati wafugaji wanahamishwa kwenda mikoa ya kusini wengine mifugo yao ilikufa njiani, lakini wafugaji kutoka Ngorongoro wamehamishwa kwa kupatiwa maeneo yenye ukubwa wa ekari tatu.
“Wamepewa ardhi ya ekari tatu, tumsaidie Rais kuwaelimisha watu umuhimu wa maeneo haya, sisi tusiwe vikwazo,” alisisitiza.
HOJA NYWELE BANDIA
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Hawa Mwaifuge, alisema kabla ya serikali kufanya uamuzi wa kupandisha kodi ya nywele bandia, ifanye utafiti kubaini idadi ya viwanda nchini vinavyozalisha nywele hizo na kwa kiwango kipi cha ubora.
Alisema uamuzi wa kupandisha kodi katika nywele hizo unaweza kuathiri maendeleo ya viwanda vya nywele nchini na kusababisha kufa badala ya kuimarika.
“Biasharayanyweleinafanywanakinamama ambao wanalipa kodi ya serikali, hawajawahi kukwepa kodi. Sisi katika viwanda vyetu tupo tayari kutengeneza wigi (nywele bandia) zenye ubora?. Tuwaache kina dada wafanye biashara, wanaleta nywele nzuri. Hii ni sekta muhimu tuache kodi kama ilivyo ili wanawake wafanye biashara vizuri,” alieleza.
Akizungumzia pendekezo la serikali kuchukua asilimia tano kati ya 10 inayotengwa na halmashauri kwa lengo la kuboresha miundombinu ya wafanyabiashara wadogo, alisema uamuzi huo utaathiri wajasiriamali.
Alisema hata asilimia 10 ya mapato ya halmashauri kutengwa kuwawezesha wajasiriamali kwa kuwapatia mikopo bado haitoshi.
“Nilitamani serikali ije na pendekezo la kuongeza asilimia 15 badala ya kupunguza asilimia 10. Tafuteni utaratibu mzuri kuhakikisha wajasiriamali wanapata maeneo yao lakini siyo kuchukua hela hizo,” alieleza.
MISAMAHA YA KODI
Mbunge wa Kinondoni (CCM) Abbas Tarimba, aliishauri serikali kuimarisha sekta zisizokuwa rasmi ili ziimarike kuwa sekta rasmi zilipe kodi kukuza uchumi wa nchi.
Pia, alisema kuna umuhimu serikali kutoa misamaha ya kodi katika maeneo yenye kumgusa mwananchi moja kwa moja na siyo maeneo ambayo hayaleti tija kwa wananchi.
“Tuliweka msamaha wa kodi kwenye simu janja lakini ziliwanufaisha wafanyabiashara, tukaweka msamaha kwenye taulo za kike zikawanufaisha wafanyabiashara. Tunaweka msamaha katika mitungi ya gesi badala ya kuweka msamaha katika gesi ambayo inawasaidia wananchi,” alieleza Tarimba.
Na MUSSA YUSUPH, Dodoma