WADAU wanane wa Mfuko wa Pamoja wa Afya, wameahidi mwaka huu wa fedha kuchangia zaidi ya sh. bilioni 98 ili kuwezesha sekta ya afya.
Kutokana na hatua hiyo, serikali imesema itahakikisha fedha zinazotolewa na wadau hao zinanufaisha jamii kwa kuwapo na huduma za uhakika, upatikanaji dawa na vifaatiba katika vituo vya afya.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, alisema mwaka wa fedha uliopita wadau hao walichangia sh. bilioni 74 na mwaka huu wameahidi kuchangia sh. biloni 98.1 ili kuwezesha sekta hiyo.
Alieleza kutokana na hatua hiyo, serikali haitakubali miradi ya afya inayowezeshwa na wadau hao ikwame, kwa sababu lengo ni kunufaisha walengwa ambao ni jamii kwa kupatiwa huduma bora.
“Hizi fedha zinafanyiwa ukaguzi na ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), nasisitiza
zitumike kwa malengo yanayokusudiwa ukiwemo ununuzi wa vifaatiba na kumaliza changamoto ambazo ni kero kwa jamii,” alisema.
Ummy alieleza zipo baadhi ya changamoto zinazolalamikiwa na wadau hao ukiwemo uratibu wa fedha hizo, kuchelewa kufikia walengwa katika vituo vya kutolea huduma na ununuzi wa vifaatiba kutofanyika ipasavyo, hivyo watendaji wanaosimamia wahakikishe wanamaliza tatizo lililopo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dk. Festus Ndugange, alisema kwa sasa serikali imejipanga kufanya mapinduzi katika ubora wa huduma za afya nchini na fedha hizo watahakikisha zinatumika ipasavyo kwa ununuzi wa vifaatiba vikiwemo vya maabara, dawa na kuwezesha huduma ya mama na mtoto kwa kuboresha wodi za kujifungulia.
“Mwaka jana walitoa sh. bilioni 74 na mwaka huu ni sh. bilioni 98, tunaahidi kuendelea kushirikiana na wadau, tutahakikisha asilimia 33 ya fedha hizi zinanunua vifaatiba ikiwemo vipimo
vya maabara ili kupunguza changamoto zilizopo,” alisema.
Alisema huduma ya mama na mtoto itafanyiwa maboresho katika vituo vyote vya afya, hususan wodi za upasuaji ambazo zitafungwa vifaa vya kisasa.
Dk. Ndugange alisisitiza haja ya ushirikishwaji wa kamati za jamii katika kupokea, kupanga, kuratibu na kusimamia vifaa vinavyonunuliwa na kudhibiti upotevu wa fedha za miradi ya afya ili kufikia lengo la kuwapo na huduma bora nchini.
Mratibu wa wadau hao wa maendeleo kutoka Ireland, Mags Gaynor, alisema ni fursa kwa wadau wanane wa maendeleo kukutana na serikali na kujadili namna ya kushirikiana kufikia lengo la kuboresha huduma za afya kuanzia ngazi ya chini ya jamii.
Alisema watahakikisha wadau wengine wanaunga mkono juhudi za pamoja na kuchangia katika mfuko huo ili kuwa na uratibu mzuri utakaopunguza changamoto zilizopo katika sekta husika.
NA MARIAM MZIWANDA