SERIKALI imesema hata kama mtumishi wa umma akiishi zaidi ya miaka 30 tangu kustaafu kwake, ataendelea kulipwa mafao yake tofauti na umri wa miaka 12.5 uliowekwa katika kikokotoo.
Pia, imesema katika majadiliano yaliyowezesha kufikia uamuzi wa kikokotoo kipya, si kweli kwamba, vyama vya wafanyakazi vilibanwa, bali vilipewa fursa pana kuwasilisha mapendekezo yao.
Msimamo huo wa serikali, ulielezwa Bungeni wakati wa mjadala wa hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali, ambapo Mbunge wa Viti Maalumu (CHADEMA), Ester Bulaya, alihoji sababu za serikali kuweka ukomo wa miaka 12.5 kwa wastaafu kuendelea kupata mafao yao.
Mbunge huyo katika mchango wake alieleza kuwa kitendo cha wastaafu kulipwa pensheni kwa miaka 12.5 baada ya kustaafu sio sahii.
“Mnamtengenezea mazingira magumu na bado mnamkadiria afe haraka kwa sababu mnajua mazingira mlioyatengeneza sio rafiki kwa wafanyakazi. Sio sawa, hawa wafanyakazi ndio wanatekeleza mipango,” alisisitiza Bulaya.
Wakati mbunge huyo akiendelea kuchangia bajeti hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako, alisimama kumuomba Naibu Spika wa Bunge, Mussa Zungu, kutaka kutoa taarifa kwa mchangiaji.
Mara baada ya Profesa Ndalichako kupewa nafasi hiyo, alisema hata kama mtumishi akiishi zaidi ya miaka 30 baada ya kustaafu, ataendelea kupata mafao yake.
“Nataka kumpa taarifa mzungumzaji (Bulaya) kwamba huo umri ambao umewekwa kwenye kikokotoo wa miaka 12.5, mtumishi ambaye Mungu akamjaalia neema ya kuishi zaidi ya miaka 30 baada ya kustaafu, ataendelea kupata mafao,” alieleza Waziri huyo.
Licha ya kupewa taarifa hiyo, mbunge huyo alikataa kuipokea kisha kuendelea kuchangia hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali ambapo alisema hata mchakato wa kufikia kikokotoo haukuwa shirikishi kwa vyama vya wafanyakazi.
Kauli hiyo ilimlazimu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, kusimama kuomba nafasi ya kumpatia taarifa mzungumzaji na alipopata fursa hiyo alisema sio kweli kwamba vyama vya wafanyakazi havikushirikishwa katika uamuzi huo.
“Naomba nimpe taarifa Ester Bulaya kwamba katika mchakato wa kufikia uamuzi wa kikokotoo, sio kweli serikali ilivibana vyama vya wafanyakazi. Tunakumbuka hata wakati wa Mei Mosi (Sikukuu ya Wafanyakazi) risala ya vyama vya wafanyakazi waliweka wazi mchakato mzima.
Aliongeza kuwa: “Walikubalina na serikali ulikuwa mchakato shirishikishi na wala haukuwa mchakato wa serikali na vya vya wafanyakazi vikabaki peke yake.”
Naye, Mbunge wa Makete (CCM), Festo Sanga, akichangia hotuba hiyo ya Bajeti Kuu ya Serikali iliyowasilishwa bungeni Juni 14 mwaka huu na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, alisema bado kuna fedha nyingi ambazo serikali haijazikusanya.
Alisema wapo Watanzania ambao wanafariki dunia wakati wakiwa na akiba ya fedha katika mitandao ya simu, mifuko ya hifadhi ya jamii na kampuni za bima lakini sheria haijaweka utaratibu wa namna gani fedha hizo zitarejeshwa.
Aliishauri serikali iunde mamlaka maalum kufuatilia fedha hizo kwani sheria iliyiopo inatambua benki pekee.
Kuhusu suala la mbolea alisema Rais Samia Suluhu Hassan ameonyesha mfano mzuri wa kutoa sh. bilioni 150 ya ruzuku ya mbolea, lakini mfumo wa manunuzi kwenye Wizara ya Kilimo umekuwa ukitoa fursa kwa mtu mmoja kupata tenda ya kunufaika.
“Waziri licha ya kufumua mfumo wa manunuzi wizarani lakini kuna dalili ya kukwama kunakosababishwa na wataalamu. Wizara ya kilimo iangaliwe kwa makini, serikali imetoa fedha nyingi lakini wapo wanasiasa na wataalamu ndani ya wizara wanamkwamisha waziri,” alieleza mbunge huyo wa Makete.
Na MUSSA YUSUPH, Dodoma