ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Dk. John Pima (44) na wenzake wawili, wamepandishwa tena kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi ikiwa na mashitaka sita.
Washitakiwa wengine ambao ni waliokuwa ni Mweka Hazina, Mariamu Mshana (43) na Mkuu wa Idara ya Mipango na Uchumi,Innocent Maduhu (40) wa halmashauri hiyo.
Dk. Pima na wenzake walisomewa mashitaka sita ya utakatishaji fedha haramu na matumizi mabaya ya nyaraka za umma, mbele ya Hakimu Mkazi, Bitton Mwakisu.
Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 5/2022, upande wa Jamhuri uliwakilishwa na Wakili wa Serikali, Charles Kagilwa, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Janeth Sekule na Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Richard Jacopiyo, huku washitakiwa wakitetewa na Mawakili Valentine Nyalu na Sabato Ngogo.
Wakili Sekule alidai kati ya Machi 23 na Mei 20, mwaka huu, washitakiwa wakiwa watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha na waajiriwa wa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), walifanya udanganyifu kwa kutumia nyaraka za uongo kwa matumizi ya sh. milioni 103, huku wakijua ni kosa kisheria.
Shtaka la pili, washitakiwa hao walidaiwa Machi 27, mwaka huu, walitumia nyaraka kwa nia ya kumdanganya mwajiri kwa kuweka nyaraka za uongo zikionyesha Maduhu ameomba masurufu ya kununua moramu na mchanga wa kutengeneza matofali, huku akijua ni kosa kisheria.
Pia, washitakiwa hao wanadaiwa Machi 27, mwaka huu, walitumia nyaraka za uongo kwa lengo la kumdanganya mwajiri kwamba kati ya Machi 28 hadi Aprili 14, mwaka huu, Maduhu aliomba masurufu kwa nia ya kujenga kiwanda cha matofali huku wakijua ni kosa kisheria.
Katika shtaka la nne, ilidaiwa washitakiwa hao Machi 27, mwaka huu, walitumia nyaraka za uongo kumdanganya mwajiri kuwa Maduhu ameomba marejesho wa masurufu inayoonyesha ametumia sh.milioni 103 kufyatua matofali.
Shtaka la tano, la utakatishaji fedha linalomkabili Maduhu anadaiwa Aprili mosi, mwaka huu, jijini Arusha alinunua gari aina ya Subaru Forester lenye namba za usajili T.844, DYY huku akijua lilikuwa zao la uhalifu.
Katika shtaka la sita la utakatishaji fedha, washitakiwa hao wanadaiwa kati ya Mei 23 na 25, mwaka huu, walijipatia sh. milioni 103, kwa kutumia nyaraka za uongo kwa kumdanganya mwajiri huku wakijua fedha hizo ni zao la uhalifu.
Washitakiwa walikana kutenda makosa hayo, ambapo upande wa Jamhuri ulidai upelelezi haujakamilika na kuomba shauri liahirishwe hadi tarehe nyingine kwa kutajwa.
Hakimu Mwakisu aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 5, mwaka huu na kuamuru washitakiwa warudishwe mahabusu kutokana na shtaka la tano na sita kutokuwa na dhamana.
KESINYINGINE YAKINADK.PIMA
Wakati huo huo, Dk. Pima na wenzake watatu jana walishindwa kukidhi vigezo vya masharti katika kesi namba tatu na nne za uhujumu uchumi zenye mashitaka manane walizosomewa Juni 17, mwaka huu.
Katika kesi hiyo, washitakiwa wengine waliokuwa watumishi wa halmashauri hiyo, Innocent Maduhu, Mkuu wa Idara ya Mipango ya Uchumi , Nuru Ginana (40) na Alex Daniel (25) wa Idara ya Mipango na Uchumi.
Washitakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo kwa dhamana, ambapo kabla ya kuanza kwa utaratibu huo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Janeth aliomba kumsomea mshitakiwa wa pili katika kesi hizo, Mariamu Mshana, mashitaka yanayowakabili kwa kuwa waliposomewa wenzake kwa mara ya kwanza hakuwepo.
Hakimu Mwakisu alimweleza mshitakiwa huyo kwamba anakabiliwa na shtaka la utakatishaji fedha ambalo halina dhamana,hivyo ataenda mahabusu hadi Julai mosi, mwaka huu, kesi hiyo itakapopelekwa kwa kusomewa maelezo ya awali.
Kuhusu dhamana za washitakiwa wengine, Wakili Nyalu anayemtetea Dk. Pima, alidai hawajakamilisha utaratibu wa dhamana, huku Wakili Ngogo wa washitakiwa Mariamu, Ginana na (Daniel) akidai kuna changamoto zilijitokeza zilizokwamisha kukamilisha utaratibu huo.
Hakimu Mwakisu aliamuru washitakiwa wote waendelee kubaki mahabusu hadi Julai mosi, mwaka huu.
Na LILIAN JOEL, Arusha