PAMOJA na ubora wa kikosi cha Yanga msimu huu ni ngumu kuacha kumtaja Kocha Nasreddine Nabi, raia wa Tunisia.
Nabi aliyetua Yanga mwaka jana uliopita, amefanya kazi kubwa na kuibadilisha timu ambayo leo hii inasherehekea na kuvuna matunda iliyopanda kupitia kocha huyo.
Kocha huyo alitua Jangwani na falsafa bora ya kuhakikisha kikosi chake kinacheza soka la pasi nyingi na kushambulia.
Moja ya silaha kubwa ya Yanga msimu huu ilikuwa umiliki wa soka katika kiungo, kasi na uwezo wa kufunga mabao mengi katika michezo iliyocheza.
Wakati anatua Yanga, inawezekana mashabiki na viongozi wa klabu hiyo hawakuwa na imani kubwa ya kubaki na kocha huyo kwa muda mrefu, lakini ubora aliouonyesha ulitosha kumbakiza.
Kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kumemfanya Nabi kuweka rekodi ya kuwa kocha wa kwanza wa timu hiyo kubeba kombe baada ya misimu minne kuambulia patupu.
Mara ya mwisho Yanga kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara ni msimu wa 2016/2017 ikiwa chini ya kocha Mzambia, George Lwandamina.
Baada ya Nabi kuipa taji Yanga, anafuata nyayo za makocha wengine akiwemo Lwandamina na Hans Pluijm ambao waliipa ubingwa wa ligi kuu timu hiyo.
Pia, kocha huyo ameifikisha Yanga katika fainali ya Kombe la FA msimu uliopita ambapo alikubali kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Simba katika Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.
Msimu huu, Nabi ameiongoza Yanga kutinga fainali ya Kombe la FA dhidi ya Coastal Union itakayochezwa katika dimba la Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
MSIMU WA MAKOMBE
Wakati akiwa na uhakika wa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, kocha huyo anaweza kuendeleza rekodi kama atafanikiwa kutwaa Kombe la FA.
Nabi anaweza kufuata nyayo za Pluijm ambaye aliipa timu hiyo ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la FA mwaka 2015/2016 akiifunga mabao 3-1 Azam FC katika dimba la Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
UBORA LIGI KUU
Yanga imekuwa na ubora mkubwa msimu huu, imetesa katika idadi ya michezo ya kushinda na kufungwa.
Timu hiyo baada ya mchezo wa juzi, imefanikiwa kuvuna pointi 73 katika michezo 29, ikishinda michezo 22 na kutoka sare michezo saba.
Miamba hiyo imekuwa timu iliyofunga mabao mengi kuliko timu yoyote msimu huu ikipachika mabao 47 na kuruhusu mabao machache zaidi (mabao saba).
WASIFU
Nabi alizaliwa mwaka 1965 nchini Tunisia na alikuja nchini Aprili 2021 na kupewa mikoba ya kuinoa Yanga.
Kwa mujibu wa mtandao, Mtunisia huyo alianza kuinoa Al Ahly SC ya Libya mwaka 2013 kabla ya mwaka huo huo kutimkia Al Hilal ya Sudan aliyodumu hadi mwaka 2014.
Msimu wa 2015-2016, Nabi aliinoa timu ya Ismaily ya nchini Misri kwa msimu mmoja.
Mwaka 2021, kocha huyo alipata kibarua katika klabu ya Al Merrikh ya nchini Sudan na mwaka huo huo Yanga ikamchukua na kuanza kukuinoa kikosi chake.
Wiki kadhaa baada ya kuachana na kocha wake, Cedric Kaze, Yanga ilimpa ajira Nabi aliyetoka Al Merrikh ya Sudan.
Kaze ambaye kwa sasa ni kocha msaidizi wa Yanga chini ya Nabi, alikuwa kocha mkuu kabla ya kuachana na timu hiyo msimu uliopita kisha kurejea tena msimu huu na kuwa msaidizi wa Nabi.
Wakati anatua Yanga, Nabi alipewa dili la kuinoa Yanga kwa miezi 18 pekee.
Na ABDUL DUNIA