WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kukuza na kutoa ushirikiano kwa mashirika yasiyo ya kiserikari (NGOs), ili kuleta tija na maendeleo kwa Watanzania.
Majaliwa amesema hayo wakati wa hafla ya chakula cha hisani iliyoandaliwa na Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote (EOTF) iliyofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.
Amesema jitihada za pamoja kati ya serikali na EOTF zinahitajika ili kuifikia jamii yote ya Tanzania kimaendeleo.
“Mafanikio hayawezi kupatikana bila ya kuungwa mkono, wadau wetu muhimu ni kama vile mashirika yasiyo ya kiserikali, wahisani kutoka sekta ya wafanyabiashara, mashirika ya maendeleo ya kimataifa, watu binafsi na madhehebu ya dini,” alisema.
Ameeleza ili kufanikisha maendeleo ya jamii, lazima watu wawezeshwe katika kuimarisha uwezo wao wa kukabiliana na changamoto zinazowazunguka kwa kubuni mbinu kuzitatua.
Waziri Mkuu aliipongeza EOTF kwa kuendelea kutoa huduma kwa Watanzania katika kipindi cha miaka 25 sasa na huduma hiyo imeleta mabadiliko kwa wananchi katika nyanja za afya, elimu na uchumi.
“Wote tumesikia kuhusu historia na kazi zilizizofanywa na EOTF na mchango mkubwa wanaoutoa kwa jamii. EOFT wanastahili pongezi nyingi sana kwa jitihada kubwa wanazozifanya ambazo leo zimeifanya taasisi hii kuwa miongoni mwa taasisi imara ambazo zimekuwa zikizaa matunda. Nami nitumie fursa hii kwa moyo wa dhati kuwapongeza kwa mafanikio yote mliyoyapata katika kipindi chote cha miaka 25,” alisema.
Waziri Mkuu alimpongeza Mwenyekiti wa EOTF, Mama Anna Mkapa na wadau wengine kwa kusimamia vyema utendaji wa taasisi hiyo ambayo imetimiza malengo ya kuanzishwa kwake.
“Nimefurahishwa sana na programu zinazoendeshwa na taasisi hii hususan programu ya “Women Business Center“(WBC) mnayoanzisha ambayo itatoa huduma za masoko, elimu ya ujasiriamali, biashara, upatikanaji wa mitaji, afya ya mama na mtoto,” alisema.
Majaliwa alieleza serikali itaendelea na jitihada za kukwamua wananchi kiuchumi kwa kutengeneza fursa mbalimbali na kutumia nyenzo za ndani kama mikopo ya asilimia 10 kwa makundi maalumu ikiwemo TASAF ili kuzisaidia kaya masikini kujikwamua.
Kwa upande wake, Mama Anna Mkapa alisema katika kuelekea awamu ya pili baada ya miaka 25, taasisi hiyo imeazimia kusonga mbele kidigitali kuwafikisha walengwa wake wanapostahili kijamii, kiuchumi, kiafya na kielimu kwa kuanzisha programu ya WBC.
Na MWANDISHI WETU