Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amechangia Tsh. Milioni 70 kwa Doris Mollel Foundation, ambapo Tsh. Milioni 20 ameitoa kuwasaidia watoto njiti kupitia shirika hilo lisilo la Kiserikali na pia amenunua vifa tiba vya kuwasaidia Watoto hao vyenye thamani ya Tsh. Milioni 50.
Akiongea katika tukio hilo, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel amemshukuru Mhe. Rais kwa kuchangia fedha hizo ambazo amezitoa mwenyewe kutoka kwenye mshahara wake, huku akiweka wazi kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Afya itaendelea kuwasaidia Watoto njiti na Wanawake wanaojifungua Watoto hao.
Nae, Mkurugenzi wa Doris Mollel Foundation ambaye pia alizaliwa Mtoto njiti, Bi. Doris Mollel amemshukuru Mhe. Rais kwa msaada huo ambapo amesema ameutoa katika siku mwafaka, ambapo Doris Mollel Foundation iliitumia siku hiyo kutoa misaada mbalimbali.
Doris Mollel Foundation huadhimisha Siku ya Mtoto Njiti Duniani ambayo kwa kawaida huadhimishwa mnamo tarehe 17 Novemba kila mwaka, Shirika la Doris Mollel Foundation liliadhimisha kilele cha siku hiyo November 20, 2022 ambayo ilikutwa Siku ya Mtoto Duniani na yalifanyika katika viwanja vya Robanda, vilivyopo katika Wilaya ya Serengeti, Mkoani Mara.