Na Oscar Assenga,TANGA.
Rais Dkt Samia Suluhu ameendelea kuiwekea historia kubwa Bandari ya Tanga kutokana na maboresho makubwa iliyoyafanya na sasa wameanza kupokea meli kubwa iliyoshusha magari kwenye Bandari hiyo
Magari hayo yalishushwa kwenye meli kubwa ya mizigo yenye urefu wa mita 179 ambayo iliweza kutia nanga katika gati lenye urefu wa mita 450 ambayo ilikuwa ikitokea nchini China na kuwa ya kwanza kuja na magari katika bandari ya Tanga tofauti na meli nyingine ambazo zilishakwisha kutia nanga bandarini hapo
Akizungumza wakati alipofanya ziara katika Bandari ya Tanga na kushuhudia ushushwaji wa magari hayo katika meli hiyo,Mkuu wa Mkoa wa Tanga Waziri Kindamba amesema ameamua kuanza ziara yake kutokana na kwamba Bandari ndio Moyo wa kiuchumi wa Tanga.
Alisema kutokana na maboresho hayo yaliyofanywa na Serikali Mkoa huo unaweza kubadilika na kuwa Califonia ya Afrika na hivyo kupelekea uchumi wetu kuendelea kuwa mzuri.
Kindamba aliwataka wafanyakazi wa Bandari kuhakikisha wanafanya kazi kwa bisi wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi kuitumia bandari ya Tanga hasa mara baada ya ukamilishaji wa ujenzi wa gati la kisasa lenye uwezo wa kuhudumia meli kubwa za mizigo tofauti na hapo awali.
Katika ziara hiyo Mkuu huyo wa Mkoa ameitambulisha rasmi kauli mbiu yake kwambq ‘Tanga lango kuu la Afrika Mashariki’.
Alisema kwamba wanaitazama bandari ya Tanga ya kimkakati zaidi huku akiwahimiza wafanyabiashara wa ndani na nje ikiwemo nchi za Afrika Mashariki kuitumia bandari ya Tanga ambayo itakuwa na manufaa makubwa kwao katika kusafirisha mizigo yao kwa haraka zaidi.
Aidha alisema kutokana na Mapinduzi makubwa yaliyofanywa na Serikali wao kama wasimamizi wataisimamia kwa ukaribu zaidi ili kuhakikisha Dunia inajua kwamba ipo bandari inayoitwa bandari ya Tanga inayofanya kazi zake kwa ufanisi mkubwa.
Awali akizungumza wakati wa ziara hiyo Meneja wa bandari ya Tanga Masoud Mrisha amemuomba Mkuu wa Mkoa kusaidia upanuzi wa miundombinu ya barabara ndani ya jiji la Tanga ili kuepusha msongamano wa magari wakati biashara itakaposhamiri bandarini hapo.
Hata hivyo alisema kwamba wanaiomba Serikali kupitia wakala wa barabara za mijini na vijijini Tarura na Tanroads kutengenezwa kwa miundombinu ya barabara inayokwenda Mwambani kwenye eneo ambalo wanatarajia kujenga sehemu ya kuhifadhia mizigo.
Meneja huyo alisema kwamba a kwa sasa wanawalika wafanyabiashara na wateja kutoka ndani na nje kuitumia bandari hiyo kutokana na maboresho makubwa yaliyofanywa na Serikali katika Bandari hiyo.
Serikali imewekeza kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 429 kwenye bandari ya Tanga kwajili ya ujenzi wa gati, kuongeza kina cha maji na ununuzi wa mitambo kwajili ya kuwezesha bandari hiyo kuhudumia meli kubwa ambazo zilikuwa zinashindwa kutia nanga bandarini hapo.