Na Mwandishi Wetu, Arusha

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT), imetoa tahadhari kwa raia wanaoshikilia fedha za kigeni hususani Dola ya
Marekani kuwa wapo katika hatari ya kupata hasara kubwa kutokana na uamuzi wao huo wakitegemea
kupata faida katika soko la fedha.
Akizungumza katika kikao kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma jijini hapa
jana, Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba, alisema Tanzania inatekeleza mikakati ya kuimarisha
upatikanaji wa Dola, hivyo kuendelea kushikilia fedha hizo kuna athari ya kupata hasara badala ya faida.
“Niwaombe (wanaoshikilia Dola), mziweke sokoni katika mfumo ulio rasmi. Tutawachukulia
hatua za kisheria wale wote watakaobainika kujihusisha na biashara haramu ya soko la fedha,”
alionya Gavana wa BoT.
Kwa mujibu wa Gavana Tutuba, upungufu wa Dola ni tatizo la kidunia lililochangiwa na
wachapishaji wa fedha hizo, Marekani, ambayo iliamua kudhibiti mfumuko wa bei kwa
kupunguza usambazaji wa Dola sokoni.



























