Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametaka kuwepo masuluhisho ya amani na uwazi kwa changamoto zozote zile zinazohusiana na uhalali wa uchaguzi wa urais wa Zimbabwe uliomrejesha madarakani Emmerson Mnangagwa.
Tume ya uchaguzi ya Zimbabwe ilisema Jumamosi kuwa Rais Emmerson Mnangagwa, ambaye ana miaka 80, alishinda kwa kupata kura takriban asilimia 52.2, wakati Nelson Chamisa mwenye umri wa miaka 45, kiongozi wa upinzani wa Citizens’ Coaliton for Change, alipata asilimia 44 ya kura.
Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres “ ana wasiwasi kuhusu kukamatwa kwa wafuatiliaji wa uchaguzi, ripoti za manyanyaso dhidi ya wapiga kura, vitisho vya ghasia, kubughudhiwa na kukandamizwa,” kulingana na msemaji wake Florencia Soto Nino.
Wakati Chimisa alisema kuwa uchaguzi ulikuwa ni wizi wa wazi na mkubwa,” Mnangagwa alisema kuwa uchaguzi ulifanyika “kwa uwazi, haki wakati wa mchana mtupu.”
Ushindi wa Mnangagwa ulikuwa ni ushindi mwingine kwa chama cha ZANU-PF ambacho kimetawala nchi hiyo tangu mwaka 1980 baada ya kupatikana uhuru kutoka utawala wa watu weupe.
Wafuatiliaji wa kimataifa wanasema uchaguzi wa wiki iliyopita katika katika taifa la kusini mwa Afrika ulifanyika katika mazingira ya hofu na vitisho.
Wapiga kura walikwenda katika vituo vya kupiga kura Jumatano na katika baadhi ya maeneo vituo vya kupiga kura vilifunguliwa siku ya Alhamisi kutokana na changamoto kadhaa za usambazaji wa karatasi za kupiga kura.
Tangazo la matokeo ya uchaguzi lililotolewa Jumamosi limekuja mapema kuliko ilivyotarajiwa.
“Sote sisi tuna maswali mengi kuhusu uharaka huu” wa kutangazwa matokeo, Nicole Beardsworth, mhadhiri wa siasa katika Chuo Kikuu cha Witwatersrand, aliiambia Reuters.
Taarifa hii ni kwa msaada wa Reuters na AP.