Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amekipongeza kiwanda cha mbolea cha ITRACOM Fertilizer Limited kwa kuzingatia sheria za kazi ikiwemo kuwapa mikataba wafanyakazi, Usalama na afya mahali pa kazi na kuwasilisha michango ya wafanyakazi kwenye mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa wakati.
Prof. Ndalichako ameyasema hayo Septemba 18, 2023 alipofanya ziara ya kutembelea kiwanda hicho kilichopo jijini Dodoma kwa lengo la kukagua utekelezaji wa Sheria za kazi, ambapo amewataka wawekezaji nchini kuiga mfano wa ITRACOM.
Waziri Ndalichako amemshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya wawekezaji nchini , uwekezaji wa kiwanda hicho cha mbolea umezalisha ajira za awali 1,198 na kitakapokamilika ajira moja za kwa moja 3500 zitazalishwa na ambazo sio za moja kwa moja zitazalishwa ajira 8000.
Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe. Jabir Shekimweri ameahidi kuendelea kuimarisha mazingira wezeshi kwa wawekezaji ili uwekezaji wa kiwanda hicho uweze kukamilika kwa wakati na kuwa na tija kwa wananchi.
Vilevile, Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Kiwanda hicho, Kimaramuziro Nkurikiye ameishukuru serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Samia kwa kuendelea kutoa ushirikiano kwenye ujenzi wa kiwanda hicho na kutatua changamoto zilizokuwa zinawakabili ikiwemo maji, Umeme, na Barabara.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akizungumza viongozi na wafanyakazi wa kiwanda cha kuzalisha mbolea Itracom Fertilizer mara baada ya kukagua utekelezaji wa sheria za kazi katika kiwanda hicho tarehe 18 Septemba, 2023 jijini Dodoma. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mhe. Jabir Shekimweri. Kulia ni Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Kiwanda cha Itracom, Kimramzilo Nkurikiye.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe. Jabir Shekimweri akieleza jambo wakati wa ziara ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana Ajira na Wenye Ulemavu) Prof. Joyce Ndalichako (hayupo pichani) wakati wa ziara yake ya kutembelea maeneo ya kazi katika Mkoani Dodoma akiambatana na Viongozi wa Taasisi zilizochini ya Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na watendaji wengine katika kiwanda cha uzalishaji mbolea Itracom Fertilizer Limited.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akisikiliza maelezo kuhusu aina ya mbolea zinazozalishwa kiwandani hapo kutoka kwa Mkurugenzi wa Idara ya Biashara na Masoko wa Kiwanda cha uzalishaji mbolea cha Intracom Fertilizer Limited Dk. Keneth Masuke (kushoto) wakati wa ziara hiyo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako (katikati) akiangalia Mchanga aina ya Phosphete unaotumika kutoa sumu kwenye udongo kabla ya kupanda mazao. Wa tatu kutoka kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe. Jabir Shekimweri.