SERIKALI Mkoani Pwani, imedhamiria kufungua Kisiwa cha Mafia katika nyanja ya Uchumi wa Bluu pamoja na kukitangaza ulimwenguni kupitia sekta ya utalii.
Aidha mkoa huo, umejipanga kukipanga kisiwa hicho, ili kuwa kisiwa kilichopangwa kimji wa kisasa lengo likiwa kuinua uchumi na pato la wilaya.
Akifungua tamasha la kisiwa cha Mafia la siku tatu linalolenga, kutangaza vivutio vilivyopo, mkuu wa mkoa wa Pwani Alhaj Abubakari Kunenge alieleza, Mafia ni kitovu cha uchumi wa bluu kati ya vivutio 82 vya utalii Mkoani humo.
“Rais Samia Suluhu Hassan anafanya kazi kubwa kulitangaza Taifa na kuvutia wawekezaji, mkoa kwa hili umejipambanua kuwa ukanda wa viwanda na sasa una viwanda 1,525 kati yake 240 ni vikubwa na vya kati”:
“Juhudi zilizopo ni kuongeza nguvu sasa katika uwekezaji wa uchumi wa bluu,Mafia imetafsiriwa vizuri kwani adhma ya Rais ni kuona uwekezaji wa uchumi wa bluu nao unakua kwa kuongeza mahoteli ya kitalii, kuongeza idadi ya watalii, kutangaza uvuvi na samaki ikiwemo papapotwe anaepatikana kisiwani hapa”anasema Kunenge.
“Tunajitahidi kuongeza watalii, kutangaza kisiwa hiki ,lakini wananchi mnapaswa kubadilika kimaisha kwa kukimbilia fursa za kibiashara,”alifafanua Kunenge.
Pamoja na hayo, Mkuu huyo wa mkoa anasema, katika kuinua uchumi wa kisiwa hicho Serikali inaweka taa uwanja wa ndege ili usafiri uwe wa muda wowote, kuongeza idadi ya ndege na kuboresha miundombinu ya usafiri.
Awali Mkuu wa wilaya ya Mafia, Zephania Sumaye alieleza Mafia kijografia imependelewa kwa kuwa na kisiwa kikubwa na vidogo.
“Kwa kuliona hili ,ndipo tulipoamua kuona haja ya kutangaza vivutio,utalii wa majini ulipo ,ili kupanua masuala ya uchumi wa bluu”alieleza Zephania.
Zephania anawaomba , wawekezaji na watalii wa ndani na wa nje ya Mafia na nchi , kwenda Mafia kujionea vivutio mbalimbali .
Akimwakilisha Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Mwenyekiti wa CCM Mkoani Pwani Mwinshehe Mlao alimpongeza mkuu wa wilaya hiyo Zephania Sumaye, kwa kuandaa tamasha hilo kubwa.
Kisiwa cha Mafia kipo wilaya ya Mafia ambayo ni kati ya wilaya Saba zilizopo Mkoani Pwani, na sio kisiwa kinachosoma Zanzibar kama baadhi ya watu wanavyodhania.